DAR-Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Kinondoni inawatafuta Alex Msama Mwita na Benny Mwita Sammoh kwa ajili ya kujibu tuhuma za kujihusisha na vitendo vya rushwa, ikiwemo kuongoza genge la uhalifu, kughushi nyaraka na kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.
Alex Msama Mwita.
Kwa mujibu wa taarifa kwa umma iliyotolewa leo Januari 22, 2026, watuhumiwa hao wanadaiwa kujipatia fedha kupitia mauzo ya kiwanja namba 33 kilichopo eneo la Vijibweni, Kigamboni jijini Dar es Salaam, kwa kutumia hati namba 129621 iliyotolewa na Kampuni ya Africa Energy Limited mwaka 2013.
Taarifa hiyo inaeleza kuwa, shauri hilo lilifunguliwa Januari 21,2026 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Hassan Makube.
Uchunguzi uliofanywa na TAKUKURU ulibaini kuwa Benny Mwita Sammoh aliwasilisha nyaraka za umiliki wa kiwanja hicho katika Baraza la Ardhi Wilaya ya Temeke, akidai kuwa amekinunua kutoka kwa Mwinyikombo Wahela, madai ambayo baadaye yalibainika kuwa si ya kweli.
Aidha, ilibainika kuwa wakati wa mchakato huo, Benny Mwita Sammoh alitumia jina jingine la Ben Samson na kufanikisha mauzo ya kiwanja hicho kwa Kampuni ya World Oil Tanzania Limited kwa kiasi cha Shilingi bilioni 1.7, huku kiasi cha Shilingi milioni 984 kikilipwa kama sehemu ya makubaliano ya mauzo.
Kati ya fedha hizo, Shilingi milioni 370 zilihamishiwa kwa Alex Msama Mwita kama sehemu ya mapato yatokanayo na mauzo hayo.



