Tunatekwa hatujui

NA LWAGA MWAMBANDE

MAANDIKO mbalimbali ya wanataaluma yanabainisha kuwa, utandawazi ni mchakato wa kuongezeka kwa muingiliano kati ya mataifa na jamii duniani katika nyanja za uchumi, utamaduni, siasa na teknolojia.
Picha na CFI.

Pamoja na faida zake, utandawazi unaweza kumteka binadamu kwa kudhoofisha uhuru wa kiuchumi, kitamaduni na kiakili.

Hili hujitokeza kupitia nguvu ya mashirika makubwa ya kimataifa, kufifia kwa tamaduni za wenyeji, utegemezi wa mifumo ya kidijitali na mashinikizo ya sera za kimataifa.

Aidha, hali hii husababisha jamii na watu binafsi kupoteza uwezo wa kufanya maamuzi huru na kulinda maslahi yao.

Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anasema ili kukabiliana na changamoto hizi, inahitajika kuimarisha elimu ya fikra huru, kuweka sera zinazolinda maslahi ya ndani, kukuza na kuhifadhi tamaduni za wenyeji, pamoja na kusimamia matumizi ya teknolojia kwa uwajibikaji.

Kwa usimamizi sahihi, utandawazi unaweza kuwa chombo cha maendeleo endelevu badala ya kuwa chanzo cha utekaji wa binadamu.Endelea;

1. Tunatekwa hatujui,
Tunategwa hatujui,
Tunashikwa hatujui,
Akili ituingie.

2. Utandawazi ni chui,
Makucha ni buibui,
Chochote hatuambui,
Akili ituingie.

3. Kama tumechanjwa ndui,
Ugonjwa hautuui,
Hadhari hatuchukui,
Akili ituingie.

4. Kama vile hatukui,
Anavyokuja adui,
Kama hatumtambui,
Akili ituingie.

5. Runinga hatuchagui?
Vishikwambi siyo tui?
Simujanja hatujui?
Akili ituingie.

6. Kaenda huko adui,
Ajua hatutambui,
Twaona hatuugui,
Akili ituingie.

7. Kamari hatuijui?
Kwani hiyo si adui?
Mkwanja hatuchagui,
Akili ituingie.

8. Ufundi hatufungui,
Na shida hatutatui,
Mkeka hatuujui?
Akili ituingie.

9. Vyakula hatuchagui,
Twaugua hatujui,
Chochote hatubagui,
Akili ituingie.

10. Hekima hatuangui,
Chini hatuzifukui,
Zaja hatuzichukui,
Akili ituingie.

11. Kwani sisi hatujui,
Na kazi hawachagui,
Wapate hawatanui?
Akili ituingie.

12. Mbona samaki huvui,
Hizo nyavu huchukui,
Kubeti hakupungui?
Akili ituingie.

13. Kwani watu hawaui,
Mapicha hawatanui,
Bunduki hawachukui?
Akili ituingie.

14. App hatuzipakui?
Na muda hazichukui?
Twaona hatuugui?
Akili ituingie.

15. Kwani picha hatujui,
Wala sisi hatukui,
Waigiza hatujui?
Akili ituingie.

16. Muda wenda hatujui,
Matunda hatutungui,
Mtego hatutegui,
Akili ituingie.

17. Vitabu hatuvijui,
Mapya hatuyazibui,
Wala hatujisumbui,
Akili ituingie.

18. Vichekesho hatujui,
Ya kwetu havitatui,
Tunacheka hatukui,
Akili ituingie.

19. Kama miti haikui,
Matunda hatuchungui,
Tunajua hatujui,
Akili ituingie.

20. Milango hatufungui,
Na vyumba hatuchagui,
Twararua kama chui,
Akili ituingie.

21. Pengine hatuugui,
Mirembe hatuijui,
Ila ndiyo hatukui,
Akili ituingie.

22. Tuyafanye yenye tui,
Na kuvaa baibui,
Ndani mtu hachungui,
Akili ituingie.

23. Joto halituchubui,
Hata tuwe chuichui,
Kwao sisi hatujui,
Akili ituingie.

24. Mpini hatuujui,
Makali hatuchungui,
Na wala hatuchagui,
Akili ituingie.

25. Anatisha hatujui,
Aja hatumchungui,
Tuko ndani ya adui,
Akili ituingie.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here