NA LWAGA MWAMBANDE
USIKU wa kuamkia leo Januari 19,2025 Senegal wameibuka mabingwa wa michuano ya Soka kwa mataifa ya Afrika (AFCON) 2025.
Ni baada ya kuwafunga wenyeji Morocco bao 1-0 katika mechi ya kusisimua ya fainaili iliyopigwa katika dimba la Prince Moulay Abdellah Stadium uliopo Rabat nchini Morocco.
Katika mtanange huo, Papa Gueye dakika ya 94 aliiwezesha Senegal kuandikisha rekodi ya kipekee katika michuano hiyo mikubwa barani Afrika.
Ushindi huo unaifanya Senegal kuendelea kujiimarisha kama moja ya mataifa yenye nguvu katika mchezo huo, huku kikosi chake kikionesha nidhamu, umoja na kiwango cha juu cha kiufundi katika mashindano yote.
Mshairi wa kisasa Lwaga Mwambande anakumbushia kuwa, ushindi wa Senegal si tu kwa Wasenegal bali ni ushindi wa Watanzania, kwani awali Timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) ilitupwa nje ya michuano hiyo baada ya kufanyiwa ndivyo sivyo wakati ikicheza na Morocco.
Ikumbukwe, Januari 4,2026 Taifa Stars ilitupwa nje ya michuano ya Kombe la Mataifa Afrika (AFCON) 2025 kufuatia kipigo cha bao 1-0 dhidi ya wenyeji, Morocco katika dimba la Prince Moulay Abdellah mjini Rabat kwenye mchezo wa hatua ya 16 bora. Endelea;
1. Mimi si Msenegali, niko na Wasenegali,
Kazi yao nzuri kweli, tena ina maadili,
Ushindi ule kamili, kuizimisha kandili,
Ushindi wa Senegali, ushindi wa Tanzania.
2. Morocco ni ndugu zetu, ina wacheza wakali,
Ila ile mechi yetu, walitupiga kuwili,
Kunyima penati yetu, ulikuwa udhalili,
Ushindi wa Senegali, ushindi wa Tanzania.
3. Tulikuwa na kisasi, tukipinga ujahili,
Soka liwe mwendo kasi, halali iwe halali,
Ilikuwa ni mkosi, kufanyiziwa akili,
Ushindi wa Senegali, ushindi wa Tanzania.
4. Hizi timu za wenyeji, zicheze kiuhalali,
Na zisizo za wenyeji, iwe haki na ukweli,
Hapo soka ni mtaji, kombe la AFCON hili,
Ushindi wa Senegali, ushindi wa Tanzania.
5. Taifa Stars ya kwetu, timu bora kwelikweli,
Tujiandae kivyetu, tuzidi kuwa wakali,
AFCON hapa kwetu, waje waona ukali,
Ushindi wa Senegali, ushindi wa Tanzania.
6. Pamoja na yote haya, AFCON nzuri kweli,
Morocco siyo wabaya, viwanja vina kibali,
Nasi twajimwayamwaya, vingine vina kivuli,
Ushindi wa Senegali, ushindi wa Tanzania.
7. Kwa sana ilipendeza, lilivyotandazwa boli,
Kasi pasi waliweza, hata kufunga magoli,
Kama kitu twajifunza, nasi tutafika mbali,
Ushindi wa Senegali, ushindi wa Tanzania.
8. Ishirini shina saba, tutambue siyo mbali,
Nchi tatu siyo haba, kwa vitendo na kauli,
Majukumu tutabeba, AFCON iwe kamili,
Ushindi wa Senegali, ushindi wa Tanzania.
9. Hongera zetu twatoa, kwa timu ya Senegali,
Kwa wenyeji kuwatoa, na figisu zao kali,
Kama mngejiondoa, hapo mngezua zali,
Ushindi wa Senegali, ushindi wa Tanzania.
10. Kuugomea mchezo, ngekuwa mbaya ajali,
Kurudi kwenye mchezo, uamuzi bomba kweli,
Sasa tuna matangazo, Bingwa wetu Senegali,
Ushindi wa Senegali, ushindi wa Tanzania.
Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602
