ACCRA-Jeshi la Polisi nchini Ghana limemkamata Nabii Evans Eshun maarufu kama Ebo Noah, baada ya utabiri wake wa kudai kuja kwa mwisho wa dunia kusababisha hofu kubwa miongoni mwa wananchi.
Nabii Eshun alidai kuwa, dunia ingeangamia siku ya Krismasi mwaka 2025 kupitia mafuriko makubwa, akieleza kuwa ni wale pekee watakaokuwa ndani ya majengo aliyoyaita “safina nane” ndio wangepona. Kauli hiyo ilizua taharuki na mjadala mpana ndani na nje ya nchi.
Kwa mujibu wa polisi, Eshun alikamatwa na Kikosi Maalumu cha Ukaguzi wa Mtandaoni chini ya Ofisi ya Inspekta Jenerali wa Polisi, kama sehemu ya juhudi za kudhibiti matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii na shughuli za mtandaoni, hususan kuelekea ibada za kidini za mkesha wa Mwaka Mpya.
Utabiri huo ulisambaa kwa kasi nchini humo kupitia mitandao ya kijamii, na kuchochea hofu, maswali na hisia kali kutoka kwa wananchi na watumiaji wa mitandao mbalimbali.
Polisi wamesisitiza kuwa,hatua zilizochukuliwa zinalenga kulinda usalama wa umma na kuzuia taarifa potofu zinazoweza kuhatarisha utulivu wa jamii. (NA)
