DODOMA-Vikao vya Kamati za Kudumu za Bunge vinatarajiwa kuanza kufanyika kuanzia Januari 13 hadi Ijumaa, Januari 23, 2026 katika Ofisi ya Bunge, jijini Dodoma.
Hayo ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kitengo cha Mawasiliano na Elimu kwa Umma cha Ofisi ya Bunge jijini Dodoma, ikieleza kuwa vikao hivyo ni sehemu ya maandalizi ya Mkutano wa Pili wa Bunge unaotarajiwa kuanza rasmi Jumanne, Januari 27, 2026.
Kwa mujibu wa ratiba hiyo, Wabunge wanatakiwa kufika Jijini Dodoma siku ya Jumatatu, Januari 12, 2026, ili kushiriki shughuli za kamati.
Katika kipindi hicho, Kamati za Bunge zinatarajiwa kutekeleza shughuli mbalimbali zikiwemo Uchaguzi wa Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti wa Kamati.
Pia Kamati kujitambulisha na kuzifahamu Wizara na Taasisi zilizo chini yake pamoja na baadhi ya sera na sheria kulingana na majukumu ya kila Kamati.
Vile vile kupitishwa kwa majukumu ya msingi ya kila Kamati na Kamati ya Bajeti kufanya maandalizi ya hoja zitakazojadiliwa na Bunge katika Mkutano wa Pili.
