Waipongeza Serikali kwa kutoa elimu ya fedha

TANGA-Wajasiriamali wadogo na wafanyabiashara jijini Tanga wameipongeza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kutoa elimu ya fedha, wakisema mafunzo hayo yamewawezesha kupata uelewa wa kina kuhusu usimamizi wa fedha binafsi, uwekaji akiba na matumizi ya mikopo salama.
Akizungumza katika mafunzo hayo yaliyofanyika katika viwanja vya Usagara jijini Tanga, mfanyabiashara Bw. Juma Bakari alisema elimu hiyo imemsaidia kutambua njia salama za kuhifadhi fedha na kuwekeza kwenye mifuko yenye faida, huku akieleza kuwa hatakopa tena mikopo isiyo rasmi maarufu kama “kausha damu”.

“Nimejua sehemu salama ya kukopa fedha na kuanzia sasa nitaachana na mikopo umiza inayohatarisha biashara zangu kwa kuwa wanadai riba kubwa. Pia nitaielimisha familia yangu kuhusu umuhimu wa kuweka akiba kwa ajili ya dharura,” alisema Bw. Bakari.
Kwa upande wa wanafunzi, vijana kutoka Chuo cha Afya Kange walioshiriki mafunzo hayo, walisema kuwa elimu ya fedha itawasaidia kutatua changamoto za usimamizi wa fedha binafsi, hususan matumizi ya mikopo ya elimu ya juu na fedha wanazopata kutoka kwa wazazi.

Mwanafunzi wa chuo hicho, Mwanahawa Haraka Mussa, alisema kupitia Wiki ya Elimu ya Fedha wamejifunza kuhusu nidhamu ya matumizi ya fedha, uwekaji akiba na matumizi sahihi ya mikopo ili kuishi vizuri wakiwa chuoni bila kuathiri masomo yao.

“Tumejifunza jinsi ya kutumia fedha, mikopo na namna ya kujiendesha kifedha katika mazingira ya chuo ili kuepuka maisha ya shida,” alisema Mwanahawa.
Akizungumza kwa niaba ya Wizara ya Fedha, Afisa Mkuu Usimamizi wa Fedha kutoka Idara ya Uendelezaji Sekta ya Fedha, Bw. Salim Kimaro, alisema lengo la maadhimisho hayo ni kufikisha elimu ya fedha kwa wananchi ili kuwawezesha kutumia kwa ufanisi huduma za kifedha zinazopatikana nchini.

Bw. Kimaro alisema mafunzo hayo yanawalenga wajasiriamali wadogo, wafanyabiashara na wanafunzi, yakijikita katika masuala ya uwekaji akiba, usimamizi wa fedha binafsi, mikopo na usajili wa vikundi vya kifedha, ili kuepuka mikopo isiyo rasmi na hatarishi.

Aliongeza kuwa tathmini ya awali inaonesha washiriki wameelewa vyema mafunzo hayo, huku baadhi yao wakianza kuwafundisha wenzao na jamii inayowazunguka, hali inayotarajiwa kuleta tija kiuchumi kwa wakazi wa Tanga na Watanzania kwa ujumla.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here