Ajali za barabarani Mjini Magharibi zaongezeka

ZANZIBAR-Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Mhe. Mohd Ali Abdalla, amesema idadi ya ajali za barabarani katika mkoa huo imeongezeka hadi kufikia ajali 80 kwa mwaka 2025, sawa na ongezeko la asilimia 6.2 ikilinganishwa na ajali 75 zilizoripotiwa mwaka 2024.
Akizungumza na waandishi wa habari katika Ofisi yake Vuga, Wilaya ya Mjini, Mhe. Abdalla amesema ajali hizo zimesababisha vifo visivyopungua 74 kwa mwaka 2025, huku mwaka 2026 ulioanza hivi karibuni tayari vifo vitano vimeripotiwa, hali inayosababisha athari kubwa kwa jamii.

Ameeleza kuwa, sababu kuu za ajali hizo ni pamoja na uchakavu wa vyombo vya moto, uzembe wa madereva na watembea kwa miguu, kutofuata sheria na kanuni za barabarani, ongezeko la vyombo vya moto pamoja na utoaji holela wa leseni katika baadhi ya maeneo.

“Kuna gari moja linaweza kupigwa faini hadi mara tano kwa siku moja, hali inayoonyesha kutokuchukuliwa tahadhari wala kutii sheria za barabarani. Mamlaka ya usafiri barabarani inapaswa kuchukua hatua kali dhidi ya magari hayo, sambamba na kusitisha bodaboda zote ambazo hazijasajiliwa kuchukua abiria,” amesema Mkuu wa Mkoa.

Aidha, amebainisha kuwa baadhi ya madereva hawapati mafunzo sahihi ya udereva kutokana na kutopitia katika vyuo vinavyotoa elimu ya udereva, hali inayochangia ajali za mara kwa mara.

Amevitaka vyombo husika kusimamia kikamilifu utekelezaji wa sheria ili kuzuia vifo vinavyoweza kuepukika.

Halikadhalika, amezitaka mamlaka husika kuandaa operesheni maalum zitakazohusisha askari wa usalama barabarani kwa lengo la kuwabaini na kuwachukulia hatua za kisheria madereva wanaokiuka sheria bila muhali.

Mhe. Abdalla pia amesisitiza Mamlaka ya Leseni na Usalama Barabarani kuwachukulia hatua kali madereva wanaorudia makosa mara kwa mara, ikiwemo kuwafutia leseni, ili kulinda maisha ya wananchi na mali zao.

Kwa upande wake, Mkuu wa Operesheni Mkoa wa Mjini Magharibi, Kamishna Msaidizi wa Polisi Bakar Suleiman Juma, amesema Jeshi la Polisi limeanzisha mfumo maalum wa kudhibiti ajali kwa kufanya operesheni ya kukamata madereva wazembe na wanaoendesha vyombo vya moto kwa mwendo kasi kuanzia tarehe 4 Februari 2026.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here