BoT yatangaza mnada wa hadhara wa uuzaji wa vifaa chakavu katika ofisi zake nchini

NA GODFREY NNKO

BENKI ya Tanzania (BoT) imetangaza kuendesha mnada wa hadhara wa uuzaji wa vifaa chakavu katika ofisi zake zilizopo mikoa ya Dodoma, Dar es Salaam, Mwanza, Arusha, Mbeya, Mtwara na Mjini Magharibi (Unguja),
Hayo ni kwa mujibu wa tangazo lililotolewa leo Februari 6,2026 na Gavana wa BoT, Emmanuel Tutuba akiwaalika wananchi wote kushiriki katika mnada huo.

Kwa mujibu wa tangazo hilo, vifaa vitakavyouzwa ni pamoja na samani za ofisi, vifaa vya ofisi, vifaa vya TEHAMA, magari, pikipiki, mitambo na vifaa vingine chakavu.

Aidha, mnada utaanza katika mikoa ya Mbeya na Mtwara tarehe 18 Februari, 2026. Kwa Dar es Salaam, mnada utafanyika kuanzia tarehe 20 hadi 22 Februari, 2026 katika maeneo mawili ambayo ni ofisi ya BoT Mtaa wa Mirambo na nyumba iliyopo Kiwanja Na. 447, Makutano ya Chole Road na Lincoln Street.

Kwa upande wa Mkoa wa Arusha na Mwanza (Capri-Point) mnada utafanyika tarehe 21 Februari 2026, wakati Mkoa wa Mjini Magharibi, Unguja utakuwa tarehe 25 Februari 2026. Mkoa wa Dodoma mnada utafanyika tarehe 26 Februari 2026, na kufungwa Mkoa wa Mwanza (tawi la BoT) tarehe 28 Februari 2026.

BoT imeeleza kuwa, mali zitauzwa kama zilivyo katika maeneo zilipo. Malipo ya vifaa chakavu yatakuwa asilimia 100, na mnunuzi atatakiwa kuondosha mali aliyonunua siku ya mnada.

Kwa magari, pikipiki na mitambo, mnunuzi atalazimika kulipa amana isiyopungua asilimia 25 ya bei na kukamilisha malipo ndani ya siku 14 kuanzia tarehe ya mnada.

Vilevile, mnunuzi atapewa siku saba kukusanya mali aliyoshinda baada ya kukamilisha malipo.

Gharama za kubadilisha umiliki wa magari, pikipiki na mitambo zitabebwa na mnunuzi kwa kufuata taratibu za kisheria.

Kwa mujibu wa tangazo hilo, ruhusa ya kuangalia vifaa itatolewa siku mbili kabla ya mnada kuanzia saa nne asubuhi hadi saa kumi jioni, huku mnada wenyewe ukianza saa nne asubuhi katika vituo vilivyotajwa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here