Burkina Faso yaja Tanzania kujifunza mageuzi ya usimamizi na uendeshaji wa Sekta ya Madini

DODOMA-Tanzania imeendelea kuimarisha na kuthibitisha nafasi yake kama kitovu cha maarifa na uzoefu katika usimamizi na uendeshaji wa Sekta ya Madini barani Afrika, baada ya kupokea Ujumbe wa kitaalamu kutoka Burkina Faso uliokuja kujifunza mifumo na mbinu bora za uendeshaji wa sekta hiyo.
Ujumbe huo ulipokelewa Februari 9, 2026, katika Ofisi za Wizara ya Madini Mtumba, Dodoma, ukiongozwa na Halidou Ouedraogo, Mshauri wa Masuala ya Uchumi, Ufuatiliaji na Tathmini kutoka Wizara ya Nishati, Madini na Machimbo (Ministry of Energy, Mines and Quarries) ya Burkina Faso.

Kwa upande wa Wizara ya Madini, mazungumzo hayo yaliongozwa na Kamishna Msaidizi wa Madini anayeshughulikia Uchimbaji Mdogo, Eng. Moses Kongola akimwakilisha Kamishna wa Madini.
Akizungumza katika kikao hicho, Eng. Kongola alieleza kwa kina mageuzi yaliyofanywa na Serikali katika kuimarisha usimamizi, urasimishaji, na uendelezaji wa wachimbaji wadogo, usimamizi wa mazingira pamoja na kuboresha mazingira ya biashara katika Sekta ya Madini.

Alibainisha kuwa Tanzania imewekeza kimkakati katika kuimarisha mifumo ya usimamizi, kuweka Sera madhubuti, Sheria na Kanuni rafiki kwa uwekezaji, pamoja na kuhamasisha uongezaji thamani wa madini ili kuongeza mchango wa sekta hiyo katika uchumi wa taifa.

Kwa upande wake, Kiongozi wa Ujumbe huo, Halidou Ouedraogo alisema Burkina Faso imevutiwa na hatua za Tanzania katika kuimarisha uwazi na uwajibikaji, kuanzisha mifumo ya kusaidia wachimbaji wadogo kuingia katika uchimbaji rasmi, na kuunganisha Sekta ya Madini na maendeleo ya uchumi wa ndani.
Aliongeza kuwa ziara hiyo inalenga kujifunza kwa vitendo ili kuboresha Sera, mifumo ya usimamizi, na mikakati ya maendeleo ya Sekta ya Madini nchini Burkina Faso.

Aidha, ujumbe wa Burkina Faso utakaa nchini kwa muda wa siku sita, ambapo pamoja na vikao vya kitaalamu na Wizara ya Madini, utatembelea mikoa na maeneo mbalimbali ya shughuli za madini ikiwemo Tabora, Kahama (Buzwagi) na Geita Gold Mine.

Ziara hizo zinalenga kuwapa wajumbe fursa ya kujifunza kwa vitendo kuhusu usimamizi wa shughuli za uchimbaji, uendeshaji wa migodi, uongezaji thamani wa madini, pamoja na mifumo ya udhibiti na usimamizi wa sekta kwa tija na uwazi.
Kikao hicho kilihitimishwa kwa pande zote mbili kukubaliana kuendelea kushirikiana, kubadilishana taarifa za kitaalamu, na kujenga ushirikiano wa muda mrefu katika masuala ya usimamizi wa rasilimali madini, hatua inayozidi kuimarisha nafasi ya Tanzania kama kituo cha rejea cha mageuzi ya Sekta ya Madini barani Afrika.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here