DAR-Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Bw. Emmanuel Tutuba, amekutana na ujumbe wa Baraza la Dhahabu Duniani (WGC) ulioongozwa na Afisa Mtendaji Mkuu, Bw. David Tait, na kujadiliana masuala mbalimbali kuhusu mpango wa ununuzi wa dhahabu wa Benki Kuu.

Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika katika Ofisi za Benki Kuu ya Tanzania jijini Dar es Salaam tarehe 13 Februari 2026, pande zote mbili zilijadili mwenendo wa utekelezaji wa mpango wa ununuzi wa dhahabu wa Benki Kuu.
Katika majadiliano hayo, Gavana alieleza kuwa, mpango huo umeendelea kutekelezwa kwa ufanisi na umeleta mafanikio makubwa katika kuimarisha akiba ya taifa. Alibainisha kuwa utekelezaji wake umevutia Benki Kuu za nchi mbalimbali barani Afrika, ambazo zimeonyesha nia ya kujifunza na kubadilishana uzoefu kuhusu namna mpango huo unavyotekelezwa na kusimamiwa.
Gavana Tutuba alisisitiza dhamira ya Benki Kuu katika kuendeleza mpango wa ununuzi wa dhahabu kama sehemu ya mkakati mpana wa kuimarisha hifadhi ya taifa ya fedha za kigeni na kuongeza uimara wa thamani ya Shilingi ya Tanzania.
Kwa upande wake, Bw. Tait ameipongeza BoT kwa mafanikio ya utekelezaji wa mpango wa ununuzi wa dhahabu, akibainisha kuwa mpango huo umeonesha matokeo chanya na umeweka mfano bora wakuigwa kwa mataifa mbalimbali duniani.
Aidha, alieleza utayari wa World Gold Council kuendelea kushirikiana na Benki Kuu katika kuimarisha urasimishaji wa wachimbaji wadogo wa dhahabu, pamoja na kutoa tafiti, takwimu na ushauri wa kitaalamu utakaosaidia katika kufanya maamuzi yenye tija, uwazi na uendelevu kwa manufaa ya sekta ya dhahabu na uchumi wa taifa kwa ujumla.





