Hakuna mgonjwa wa UVIKO-19,mafua makali na kipindupindu Tanzania-Waziri Mchengerwa

DAR-Wizara ya Afya imewataka wananchi kuendela kuchukua tahadhari na kufuatilia ushauri wa kitaalam ili kujikinga dhidi ya magonjwa mbalimbali kama ilivyoelezwa katika taarifa kwa umma ya Mganga Mkuu wa Serikali hivi karibuni.
Hayo yamebainishwa leo Februari 27, 2026 Jijini Dar es salaam na Waziri wa Afya Mhe. Mohamed Mchengerwa alipofanya ziara ya kimakakati katika hospitali ya Rufaa Mkoa Amana kwa lengo la kukagua utolewaji wa huduma za afya pamoja na maendeleo ya uboreshaji wa miundombinu ya hospitali hiyo.

Aidha amesema, Serikali bado inaendelea kufuatilia kwa ukaribu juu ya mienendo ya magonjwa mbalimbali kama kipindu pindu, Dengue na UVIKO-19 hususani katika kipindi hiki cha mvua huku akisistiza kwamba hakuna kisa chochote UVIKO, cha mgonjwa aliyelazwa katika hospitali nchini.

“Napenda kuwahakikishia wananchi na Watanzania wote Serikali yenu ipo makini na inaendelea kufuatilia kwa karibu mwenendo wa maambukizi ya UVIKO-19 nchini na kimataifa, lakini pia tunasisitiza umuhimu wa kila mmoja kuendelea kuchukua tahadhari na kuzingatia ushauri wa kitaalamu unaotolewa na wataalamu wa afya ili kulinda afya binafsi na ya jamii kwa ujumla,” amesema Mhe. Mchengerwa.

Mhe. Mchengerwa amewataka Watanzania kujiandikisha na kulipia bima ya afya kwa wote sababu gharama za matibabu zinaweza kuwa kikwazo kwa wananchi wa hali ya chini hasa wanapohitaji kufanyiwa huduma za kibingwa na kibingwa bobezi.

Waziri Mchengerwa amesema kuwepo kwa bima ya afya kwa wote kuendana sanjari na upatikanaji wa dawa katika vituo vya afya na hospitali ili kukamilisha dhamira ya serikali katika kurahisisha huduma za afya kwa wananchi.

Katika ziara hiyo, Mhe. Mchengerwa ameambatana na Katibu Mkuu Dkt. Seif Shekalaghe pamoja na menejimenti ya Wizara ya Afya, ambapo alikagua hali ya upatikanaji wa huduma, kusikiliza changamoto zinazowakabili watumishi na wagonjwa, na kueleza mikakati madhubuti ya serikali katika kuimarisha ubora na ufanisi wa huduma za afya kwa wananchi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here