Jeshi la Polisi lafunguka madai ya kutekwa kwa Mchungaji Yanick Mbombo Cele jijini Dar es Salaam

NA DIRAMAKINI

JESHI la Polisi limetoa ufafanuzi kuhusu taarifa zinazosambaa katika mitandao ya kijamii zikidai kuwa, Mchungaji Yanick Mbombo Cele ametekwa na watu wasiojulikana jijini Dar es Salaam, likisisitiza kuwa linaendelea na uchunguzi wa kina kubaini ukweli wa taarifa hizo.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Msemaji wa Jeshi la Polisi makao makuu jijini Dodoma, mchungaji huyo, raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, aliwahi kukamatwa mkoani Iringa Mei 15, 2025, akikabiliwa na tuhuma mbalimbali ikiwemo ubakaji na mauaji ya watoto wadogo, pamoja na vitendo vya utapeli kwa njia ya kujipatia fedha kutoka kwa waumini wake kwa madai ya kuwaponya au kuwafanyia maombi maalum.

Taarifa hiyo inaeleza kuwa,uchunguzi wa awali ulibaini kuwepo kwa mtandao wa vitendo vya kihalifu uliodaiwa kuendeshwa na mchungaji huyo kwa kushirikiana na wenzake.

Aidha, upekuzi uliofanyika nyumbani na katika kanisa lake uliwezesha kupatikana kwa vielelezo mbalimbali vilivyosaidia katika uchunguzi.

Baadaye, tarehe Juni 17, 2025, mchungaji huyo pamoja na wenzake watano walifikishwa mahakamani na kusomewa mashitaka ya kuendesha genge la uhalifu na kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.

Hata hivyo, ushahidi kuhusu tuhuma za mauaji na ubakaji haukukamilika kwa kiwango cha kuweza kuwashtaki kwa makosa hayo, hivyo washitakiwa waliendelea kujibu mashitaka mengine yaliyowasilishwa mahakamani.

Julai 14, 2025, Mahakama ilitoa hukumu baada ya washtakiwa kukiri makosa kwa njia ya makubaliano (plea bargaining), ambapo walihukumiwa kutumikia kifungo cha miezi 12, kulipa faini ya Shilingi milioni 20 na magari matatu yaliyotumika katika shughuli hizo kutaifishwa. Baada ya kulipa faini, waliruhusiwa kwa mujibu wa sheria.

Jeshi la Polisi limeeleza kuwa,licha ya hukumu hiyo, taarifa zaidi zilijitokeza zikidai kuwa mchungaji huyo aliendelea kujihusisha na vitendo vya udanganyifu kupitia kanisa lake la Ebenezer Restoration Ministry for All Nations, hali iliyopelekea kukamatwa tena na kuwekwa chini ya ulinzi kwa uchunguzi zaidi.

Aidha, ilibainika kuwa alikuwa akiishi nchini kinyume cha sheria baada ya kuingia bila kibali halali, na hatua za kumrudisha kwao zilichukuliwa.

Kuhusu madai ya kutekwa, Polisi wamesema wanafuatilia kwa karibu taarifa hizo na wamewataka wananchi wenye taarifa au ushahidi wowote unaoweza kusaidia kuthibitisha au kukanusha madai hayo, kufika katika kituo chochote cha Polisi kilicho karibu nao.

Jeshi la Polisi limetoa wito kwa wananchi kuendelea kuwa watulivu na kuepuka kusambaza taarifa zisizothibitishwa, huku likiahidi kuendelea kulinda usalama wa raia na mali zao kwa mujibu wa sheria.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here