ATCL yaomba radhi kuchelewa kwa safari ya ndege Dar kwenda Mwanza

DAR-Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) limesema hali mbaya ya hewa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwanza ilisababisha kuchelewa kwa safari ya ndege TC102 kutoka Dar es Salaam kwenda Mwanza, baada ya rubani kushindwa kutua mara mbili kwa sababu za kiusalama.
Katika taarifa iliyotolewa Jumapili, ATCL ilieleza kuwa ndege aina ya Boeing 737-9 MAX iliondoka katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) saa zilizopangwa, ikiwa na abiria 165. Hata hivyo, ilipokaribia Mwanza, hali ya hewa ilibainika kuwa haikuwa salama kwa kutua.

Kwa mujibu wa taratibu za usalama wa anga, rubani alifanya majaribio mawili ya kutua bila mafanikio, kabla ya kuwasiliana na mamlaka za uongozaji ndege na kuamua kuielekeza ndege hiyo katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) kusubiri hali ya hewa kuimarika.

Ndege ilitua salama KIA na kukaa hapo kwa takribani saa tatu na nusu. ATCL ilisema uamuzi huo ulifanywa kwa kuzingatia vigezo vya kimataifa vya usalama wa safari za anga, huku usalama wa abiria ukipewa kipaumbele cha juu.

Baada ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania kuthibitisha kuimarika kwa hali ya hewa katika Uwanja wa Ndege wa Mwanza, ndege iliondoka KIA kuelekea Mwanza na kutua salama majira ya saa 11:24 alfajiri.

Hakuna majeruhi wala hitilafu ya kiufundi iliyoripotiwa. ATCL iliongeza kuwa ilitoa huduma kwa abiria wote waliokuwa ndani ya ndege wakati wa kusubiri, kwa mujibu wa taratibu za kampuni.

Shirika hilo limeomba radhi kwa usumbufu uliosababishwa na kuchelewa kwa safari hiyo na kusisitiza kuwa maamuzi yote yalifanywa kwa maslahi ya usalama wa abiria na wafanyakazi wa ndege.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here