NA DIRAMAKINI
JESHI la Mexico limetangaza kumuua kiongozi wa moja ya magenge hatari zaidi ya uhalifu wa kupangwa nchini humo, katika operesheni maalum ya kijeshi iliyofanyika Jimbo la Magharibi la Jalisco.
Kwa mujibu wa taarifa rasmi ya Wizara ya Ulinzi ya Mexico, vikosi vya usalama vilimlenga Nemesio Ruben Oseguera Cervantes, maarufu kwa jina la utani “El Mencho”, ambaye alikuwa akiongoza kundi la Jalisco New Generation Cartel (CJNG).
Operesheni hiyo ilitekelezwa siku ya Jumapili katika eneo la Tapalpa, lililoko takribani saa mbili kwa gari kusini-magharibi mwa mji wa Guadalajara, katika jimbo la Jalisco.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, vikosi vya jeshi vilianzisha operesheni maalum ya kumkamata Oseguera Cervantes kufuatia taarifa za kijasusi zilizobaini uwepo wake katika eneo hilo la milimani.
Aidha,wakati wa jaribio la kumtia mbaroni, mapambano yalizuka kati ya wanajeshi na walinzi wa kiongozi huyo wa genge hatari la dawa za kulevya.
Katika makabiliano hayo, Oseguera Cervantes alijeruhiwa vibaya. Serikali ilieleza kuwa, alifariki dunia akiwa njiani kwa ndege akipelekwa jijini Mexico City kwa matibabu ya dharura.
Wizara ya Ulinzi ilisisitiza kuwa, operesheni hiyo ilikuwa sehemu ya mkakati mpana wa serikali wa kupambana na uhalifu wa kupangwa na mitandao ya biashara haramu ya dawa za kulevya ambayo imekuwa ikiathiri usalama wa taifa hilo kwa miongo kadhaa.
Kifo cha “El Mencho” kinachukuliwa kuwa pigo kubwa kwa CJNG, moja ya makundi yenye ushawishi na nguvu kubwa katika biashara ya dawa za kulevya barani Amerika ambalo liliasisiwa mwaka 2009.
Kundi hilo limekuwa likihusishwa na usafirishaji wa dawa za kulevya kwenda nchini Marekani, vitendo vya kigaidi dhidi ya maafisa wa usalama, pamoja na upanuzi wa mtandao wake kimataifa.
Wachambuzi wa masuala ya usalama wanaona kuwa kuondolewa kwa kiongozi huyo kunaweza kubadilisha mwelekeo wa mapambano dhidi ya magenge ya dawa za kulevya nchini Mexico.
Hata hivyo, wapo wanaonya kuwa hatua hiyo inaweza pia kusababisha mivutano ya ndani ya kundi hilo au kuibuka kwa makundi pinzani yanayowania madaraka, jambo linaloweza kuongeza machafuko ya muda mfupi katika maeneo yanayodhibitiwa na kundi hilo.
Mexico imekuwa ikikabiliwa na changamoto kubwa ya uhalifu wa kupangwa, huku operesheni za kijeshi dhidi ya makundi ya magenge ya dawa za kulevya zikiendelea kuibua mjadala kuhusu athari zake kwa haki za binadamu na usalama wa raia.
Serikali imekuwa ikiahidi kuimarisha ushirikiano wa kiintelijensia na taasisi za kimataifa ili kukomesha mtandao wa biashara haramu unaovuka mipaka.
Tukio hili linaashiria hatua muhimu katika juhudi za mamlaka za Mexico za kudhibiti nguvu ya magenge hatari ya dawa za kulevya, huku macho ya jamii ya kimataifa yakielekezwa kuona iwapo litachochea kupungua kwa viwango vya uhalifu au kuibua sura mpya ya migogoro ya makundi ya kihalifu nchini humo.
Kundi la Jalisco New Generation Cartel (CJNG) ni miongoni mwa magenge ya dawa za kulevya yenye nguvu na kasi kubwa ya ukuaji katika ulimwengu wa uhalifu wa kupangwa nchini Mexico.
Aidha,likiwa limeanzishwa mwaka 2009, kundi hilo limejijengea sifa ya ukatili, ubunifu wa kivita na mtandao mpana wa kimataifa unaolivusha mipaka ya taifa hilo hadi Marekani.
Hivi karibuni,utawala wa Rais wa Marekani, Donald Trump uliitambua CJNG kama kundi la kigaidi la kigeni, hatua iliyoashiria kuongezeka kwa wasiwasi wa Washington kuhusu ushawishi na athari za kundi hilo katika usalama wa ndani wa Marekani.
Uamuzi huo uliipa mamlaka ya Marekani nyenzo pana zaidi za kisheria na kiusalama za kukabiliana nalo.
Rais wa Mexico Claudia Sheinbaum, kama ilivyokuwa kwa mtangulizi wake, amekuwa mkosoaji wa mkakati wa zamani wa “kuwawinda vinara” wa dawa za kulevya.
Mkakati huo uliolenga kuwaondoa viongozi wakuu wa magenge ulionekana mara nyingi kusababisha mgawanyiko wa makundi na milipuko mipya ya vurugu kadri makundi madogo yalivyoibuka kupigania madaraka.
Ingawa Sheinbaum anaendelea kuwa na umaarufu miongoni mwa raia wa Mexico, suala la usalama limebaki kuwa changamoto sugu.
Tangu Rais Trump arejee madarakani mwaka mmoja uliopita, serikali ya Mexico imekuwa chini ya shinikizo kubwa kuonesha matokeo dhahiri katika vita dhidi ya biashara ya dawa za kulevya na magenge yanayovuka mipaka.
CJNG imejipambanua kwa mashambulizi makali dhidi ya vikosi vya usalama, yakiwamo mashambulizi dhidi ya helikopta za kijeshi.
Pia, kundi hilo limekuwa miongoni mwa waanzilishi wa matumizi ya ndege zisizo na rubani (drones) kurusha vilipuzi pamoja na kutega mabomu ardhini, mbinu zinazoongeza hatari kwa wanajeshi na raia kwa ujumla.
Mwaka 2020, kundi hilo lilihusishwa na jaribio la mauaji lililotikisa taifa, lililotekelezwa katikati ya jiji la Mexico City, likihusisha maguruneti na bunduki zenye nguvu kubwa.Shambulio hilo lilimlenga aliyekuwa mkuu wa polisi wa jiji hilo, ambaye kwa sasa ni waziri wa usalama wa shirikisho.
Kwa mujibu wa Mamlaka ya Kupambana na Dawa za Kulevya ya Marekani (DEA), CJNG inachukuliwa kuwa na nguvu zinazokaribiana na zile za Sinaloa Cartel, mojawapo ya makundi ya uhalifu yenye sifa mbaya zaidi nchini Mexico. Inadaiwa kuwepo katika majimbo yote 50 ya Marekani.
CJNG ni miongoni mwa wasambazaji wakuu wa Cocaine katika soko la Marekani na, sawa na Sinaloa, huingiza mabilioni ya dola kupitia uzalishaji na usambazaji wa fentanyl pamoja na methamphetamine, dawa ambazo zimechangia pakubwa katika janga la uraibu na vifo vinavyotokana na dawa za kulevya nchini Marekani.
Hata hivyo, Sinaloa Cartel imeonekana kudhoofishwa na migogoro ya ndani kufuatia kupoteza viongozi wake wakuu, akiwemo Ismael Zambada Garcia maarufu kama “El Mayo”, na Joaquin Guzman maarufu kama “El Chapo”, ambao kwa sasa wanazuiliwa nchini Marekani. (NA)
