Katibu Mkuu Shelukindo ateta na Mkurugenzi wa IAEA

DODOMA-Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Dkt. Samwel William Shelukindo, amekutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi wa Idara ya Afrika wa Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki (IAEA), Bw. Gashaw Wolde, katika kikao kilichofanyika Februari 2, 2026, jijini Dodoma.
Akizungumza wakati wa kikao hicho, Balozi Shelukindo alimkaribisha Bw. Wolde nchini Tanzania, na kueleza kuwa ziara hiyo ni ishara ya uhusiano mzuri uliopo kati ya Tanzania na IAEA ambapo alisisitiza kuwa Tanzania imeendelea kunufaika na ushirikiano huo katika sekta ya afya, kilimo, maji, mazingira, nishati na viwanda.
Amefafanua kuwa, ushirikiano huo umeiwezesha Tanzania kutumia teknolojia ya nyuklia kwa amani, katika kuboresha huduma za afya hususan katika uchunguzi na matibabu ya saratani, kuimarisha usalama wa chakula kupitia maabara za kisasa, pamoja na kuendeleza mifumo ya usalama, ulinzi na udhibiti wa mionzi kwa kuzingatia viwango vya kimataifa.
Balozi Shelukindo, amebainisha kuwa Tanzania, kwa kushirikiana na IAEA, imejijengea nafasi ya kuwa kitovu cha utaalam wa sayansi ya nyuklia katika Ukanda wa Afrika Mashariki, kupitia taasisi za elimu ya juu kama Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela, ambazo zimekuwa zikitoa mafunzo ya kitaalam katika fani ya fizikia ya tiba na nyanja nyingine za sayansi ya nyuklia.

Katika sekta ya nishati, Balozi Shelukindo alisema kuwa IAEA imeendelea kuiunga mkono Tanzania, katika kupanga na kujiandaa kwa muda mrefu kuhusu matumizi ya nishati ya nyuklia kama sehemu ya mkakati wa mseto wa vyanzo vya nishati, huku akisisitiza dhamira ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuendelea kudumisha na kuimarisha ushirikiano uliopo na IAEA.

Kwa upande wake, Bw. Gashaw Wolde aliipongeza Tanzania kwa matumizi bora na ya amani ya teknolojia ya nyuklia, na kuahidi kuwa IAEA itaendelea kushirikiana na Serikali katika kuunga mkono vipaumbele vya maendeleo ya taifa.
Kikao hicho kimefanyika kufuatia ziara ya Bw. Wolde nchini Tanzania, inayofanyika kuanzia tarehe 2 hadi 6 Februari 2026, ikiwa na lengo la kuimarisha ushirikiano wa muda mrefu kati ya Tanzania na IAEA katika matumizi ya sayansi na teknolojia ya nyuklia kwa madhumuni ya amani na maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here