NA FAUSTINE KAPAMA
Mahakama Dodoma
MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Emmanuel John Nchimbi, leo tarehe 02 Februari, 2026 amewaongoza Watanzania kuadhimisha Siku ya Sheria nchini, akimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe Dkt. Emmanuel John Nchimbi, akiwasili katika Viwanja vya Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania kwa ajili ya maadhimisho ya Siku ya Sheria, leo tarehe 2 Februari, 2026.
Meza Kuu ikishiriki kuimba Wimbo wa Taifa na Wimbo wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Hii ni mara ya kwanza kwa Makamu wa Rais Tanzania kushiriki kwenye Maadhimisho ya Siku ya Sheria tangu kuanzishwa mwaka 1997.
Mhe. Dkt Nchimbi aliwasili katika Viwanja vya Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania, Tambukareli majira ya saa 3:25 hivi asubuhi na kupokelewa na mwenyeji wake, Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. George Masaju, pamoja na Viongozi wa Mahakama na Serikali.
Baada ya kufika jukwaa kuu, Wimbo wa Taifa na wa Afrika Mashariki ulipigwa kabla ya Mshereheshaji Mkuu kwenye maadhimisho hayo, Hakimu Mkazi, Mhe. Mutandzi Akiza Matovelo, kuwakaribisha Viongozi wa Dini kuyaweka maadhimisho hayo mbele za Mungu.
Majaji wa Mahakama ya Rufani na Mahakama Kuu ya Tanzania na Wegeni mbalimbali wakishiriki kuimba Wimbo wa Taifa.
Sehemu ya Wageni waalikwa wakiimba Wimbo wa Taifa na ule wa Afrika Mashariki.
Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Eva Nkya, akitoa utambulisho wa wageni mbalimbali waliohudhuria maadhimisho hayo.
Kwaya ya Mahakama ya Tanzania, Ng'aring'ari, ikiwa katika ubora wake (juu na picha mbili chini).
Kilichofuata baada ya hapo ni utambulisho wa Viongozi na Wageni mbalimbali waliohudhuria maadhimisho hayo. Utambulisho huo ulifanywa na Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Eva Nkya.
Baada ya utambulisho, kikundi cha Ngoma cha Nyota kilitumbuiza na kuteka jukwaa, kiasi cha kuwafanya Viongozi na Wageni waalikwa kuacha viti vyao na kwenda kuserebuka na kuwapongeza wanakikundi hao kwa burudani safi.
Kumalizika kwa burudani hiyo kulimpa nafasi Mshereheshaji Mkuu kuanza kuita Viongozi mbalimbali kutoa salamu. Aliyekuwa wa kwanza ni Rais wa Chama cha Mawakili Tanganyika [TLS], Boniface Mwabukusi, akifuatiwa na Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mhe. Samweli Maneno, ambaye alimwakilisha Mwanasheria Mkuu wa Serikali [AG].
Kabla ya Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania kupanda jukwaani kuzungumza na Watanzania, Mshereheshaji Mkuu katika maadhimisho hayo alikaribisha Kikundi cha Kwaya ya Mahakama maarufu Ng’aring’ari ambacho kilikonga nyoyo za wananchi waliokuwa wamefurika katika Viwanja vya Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania.
Baadhi ya Viongozi, akiwemo Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima na wananchi wengine walishindwa kujizuia, wakaamua kuachia viti vyao na kuwatunza waimbaji hao kufuatia burudani safi ya nyimbo iliyokuwa inatolewa na kwaya hiyo.
Wimbo maalumu wa Kwaya ya Mahakama, hususan unaoelezea kauli mbiu ya maadhimisho ya Siku ya Sheria mwaka 2026 umewaacha Wananchi wakitabasamu muda wote kutokana na ujumbe bora na burudani safi iliyokuwa inatolewa.
Baada ya wimbo huo, Jaji Mkuu alizungumza na Wananchi wakati wa maadhimisho hayo na baadaye kumkaribisha Makamu wa Rais kuzungumza na Taifa, kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Katika kukamilisha maadhimisho hayo ya Siku ya Sheria yanayoashiria mwaka mpya wa shughuli za kimahakama, Jaji Mkuu wa Tanzania amekagua gwaride maalumu lililokuwa limeandaliwa na Jeshi la Polisi kwa heshima yake na kwa ajili ya shughuli hiyo.
Maadhimisho hayo yaliyofanyika Kitaifa katika Viwanja vya Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini hapa yamehudhuriwa na Viongozi mbalimbali wa Mahakama, akiwemo Majaji wa Mahakama ya Rufani.
Alikuwepo pia Jaji Mkuu wa Zanzibar, Mhe. Khamis Ramadhan Abdalla, Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani, Majaji wa Mahakama Kuu, Mtendaji Mkuu wa Mahakama, Prof. Elisante Ole Gabriel na Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Eva Kiaki Nkya.
Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mhe. Samweli Maneno akitoa salamu kwenye maadhimisho hayo.
Rais wa Chama cha Mawakili Tanganyika [TLS], Boniface Mwambukusi, akitoa salamu kwenye maadhimisho hayo.Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. George Masaju, akikagua gwaride lililokuwa limeandaliwa na Jeshi la Polisi kwa heshima yake na kiashirio cha kuanza mwaka mpya wa shughuli za kimahakama, 2026.
Wageni wengine walikuwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Mussa Azzan Zungu, Mawaziri mbalimbali wakiongowa na Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Juma Homera, Manaibu Waziri, Makatibu Wakuu, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, wawakilishi wa Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama, Wakuu wa Wilaya, Viongozi wastaafu wa Mahakama na Serikali, Rais wa Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS), Bw. Boniface Mwabukusi na Wananchi kwa ujumla.
Viongozi wengine waliohudhuria maadhimisho hayo ni Makamishna wa Tume ya Utumishi wa Mahakama, Katibu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Baraka Leonard, Rais wa Mahakama ya Afrika Mashariki, Mhe. Nestory Kayobera, Menejimenti ya Mahakama ya Tanzania, Viongozi wa Mahkama Zanzibar, Mkurugenzi wa Mashtaka, Wakili Mkuu wa Serikali, Viongozi wa Dini na Mila na Wakuu wa Taasisi mbalimbali za umma.
Maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini hufanyika kila mwaka kuashiria mwanzo wa shughuli za kimahakama kwa mwaka husika. Hufanyika kwenye kila Kanda ya Mahakama Kuu, Mikoa na Wilaya zote nchini.











