JAMES BUSANYA,
ARAPHA RUSHEKE
Mahakama Dodoma
RAIS wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Wakili Msomi Boniface Mwabukusi, leo tarehe 02 Februari, 2026 ameipongeza Mahakama ya Tanzania kwa maboresho mengi ambayo yamefanyika, akitoa salamu katika maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini, amesema chama hicho kinatambua na kupongeza jitihada kubwa zilizokwisha fanyika na zinazoendelea kufanywa na Mahakama ya Tanzania.

Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) Wakili Msomi Boniface Mwabukusi leo tarehe 02 Februari,2026 akitoa hotuba kwa niaba ya Chama hicho wakati wa Sherehe za kilele cha kuadhimisha siku ya sheria nchini zikiashiria kuanza kwa mwaka wa kimahakama, zilizofanyika kitaifa katika viwanja vya Makao makuu ya Mahakama jijini Dodoma.
Akizungumza katika kilele cha kuadhimisha Siku ya sheria nchini zikiashiria kuanza kwa mwaka wa kimahakama zilizofanyika katika viwanja vya Makao Makuu ya Mhakama yaliyopo Jijini Dodoma Wakili Mwabukusi amesema jitihada hizo ni za kipekee na wanajivunia jitihahada hizo.
Aidha, akizungumzia kauli mbiu siku ya sheria Nchini 2026 inayosema, mchango wa mahakama katika ustawi na maendeleo ya Taifa akieleza kufurahishwa kwake na kauli mbiu ya mwaka huu ambayo imebeba uzito mkubwa unaodhihirisha ukweli kuwa hakuna maendeleo ya kweli bila haki
“Kauli mbiu hiyo inaakisi umuhimu wa kuweka maslahi ya wananchi mbele bila upendeleo, huku akisisitiza kuwa katika kutekeleza jukumu lake la kikatiba, Mahakama imeendelea kutoa haki kwa uwazi, bila upendeleo na kwa wakati ili kuwawezesha wananchi kuendelea na shughuli zao za kimaendeleo,”amesema Rais wa TLS.
Wakili Mwabukusi amesisitiza umuhimu wa Taasisi za Umma ikiwemo Mahakama, Jeshi, Wizara na Taasisi nyingine kufanya kazi kwa uwazi na uwajibikaji kwa manufaa ya umma.
Vilevile, aliendelea kusema kwamba TLS inaamini katika kulinda uhuru na usalama wa Mawakili katika utekelezaji wa majukumu yao ya kitaaluma, hususani wanapowatetea wateja wanao tuhumiwa kwa makosa mbalimbali mfano, wizi, ubakaji, ufisadi na mengineyo, akisisitiza kuwa wakosaji wana haki ya kuwakilishwa kisheria na Mawakili hao wasihusishwe na tuhuma za wateja wao.
Aidha, ameiomba Serikali kuona umuhimu wa kushirikisha TLS katika mchakato wa uandaaji wa miswada na marekebisho ya sheria, akieleza kuwa ushirikishwaji huo utasaidia kuboresha mfumo wa sheria nchini.
Sehemu ya Wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Wasichana Msalato wa walioshiriki sherehe za kilele cha kuadhimisha siku ya sheria nchini.Rais huyo wa TLS amesema Chama hicho kinaendelea kuhimiza uwajibikaji wa wanasheria katika majukumu yao na kusisitiza kuwa uwakili ni taaluma ya kuhudumia wananchi.
Ameeleza kuwa TLS kupitia Ofisi zake nchini kote imetoa huduma za msaada wa kisheria kwa wananchi 421 ambao 270 wanaume na 151 ni wanawake, kupitia mfuko unaofadhiliwa na michango ya mawakili wanachama wa TLS. Pia, kupitia ushirikiano wake na Wizara ya Katiba na Sheria, TLS imewafikia wananchi 3,662,643 kwa huduma mbalimbali za kisheria.
Kutokana na ufinyu wa rasilimali fedha, Wakili Mwabukusi ameiomba Serikali kutenga fungu maalum la kusaidia wananchi wenye uhitaji wa msaada wa kisheria ili TLS iweze kuwafikia wananchi wengi zaidi na kuleta usawa katika upatikanaji wa haki.
Amesema TLS ipo tayari kushirikiana na wadau wote wa maendeleo ya Sekta ya Sheria, akibainisha kuwa katika ushauri watashauri, katika mema watapongeza na pale panapohitaji kukemewa watakemea.
Sehemu ya watumishi wa Mahakama ya Tanzania walioshiriki sherehe za kilele cha kuadhimisha siku ya sheria nchini.
Amepongeza matumizi ya njia mbadala za utatuzi wa migogoro (ADR) kupitia Mahakama, akisema hatua hiyo imechangia kupunguza msongamano wa mashauri mahakamani.
Aidha, amegusia changamoto ya kutooana kwa mifumo ya vyombo vinavyoshughulikia masuala ya nyumba, ardhi na Mahakama, akisema wingi huo unaleta mkanganyiko na ni vyema kupunguza utitiri huo kwa ufanisi zaidi.
Wakili Mwabukusi ameeleza tofauti za mifumo ya utoaji haki kati ya Zanzibar na Tanzania Bara, akitoa mfano kuwa Zanzibar mtuhumiwa akikaa mahabusu zaidi ya miezi sita hupata dhamana, tofauti na Tanzania Bara kwa baadhi ya makosa yasiyo na dhamana. Ameishauri Serikali kuangalia uwezekano wa kutoa dhamana katika mazingira kama hayo ili kuleta usawa.
Pia amesisitiza umuhimu wa kuimarisha Shule ya Sheria kwa Vitenda (Law School of Tanzania) kwa kuweka chujio madhubuti la kitaaluma na kimaadili ili kupata Mawakili wenye sifa stahiki, akisema si lazima kila Msomi wa Sheria awe Wakili.
Makamu wa Rais ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimu Balozi Dkt. Emanuel Nchimbi (wa nne kulia) akifuatilia kwa umakini hotuba ya Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) wakili Msomi Boniface Mwabukusi.Aidha, ameishauri Serikali kuongeza bajeti kwa ajili ya kuongeza idadi ya Mawakili wa Serikali ili kuimarisha utoaji wa huduma za kisheria serikalini.
Wakili Mwabukusi ametoa pongezi kwa Mahakama ya Tanzania kwa maboresho makubwa ya miundombinu na matumizi ya TEHAMA, pamoja na juhudi za kufuatilia haki ya dhamana katika mahakama za mwanzo ili kuwawezesha wananchi kupata dhamana kwa mujibu wa sheria.
Amehitimisha kwa kusisitiza umuhimu wa usawa mbele ya sheria, uwazi katika uwasilishaji wa vielelezo vya ushahidi kuwapa fursa upande wa pili kutambua na kuvifanyia kazi na kuhimiza mshikamano katika kuendeleza haki, usawa na ustawi wa maendeleo kwa wote.
