DAR-Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam,Mheshimiwa Albert Chalamila amemaliza mgogoro uliodumu kwa takribani miaka 15 katika eneo la Kariakoo ukihusisha familia ya marehemu Abdallah Sultani Mtambo akiwemo aliyekuwa mkewe Bi.Malaya Mtambo na Salim Selemani Salim ambaye alinunua nyumba hiyo namba 12 kiwanja namba 15 kupitia mnada wa Mahakama, ambapo amemkabidhi Salim Selemani Salim kama mmiliki halali aliyeinunua nyumba hiyo kihalali.

Akizungumza Februari 17,2026 jijini Dar es salaam mara baada ya kusikiliza taarifa ya kamati aliyoiunda alipotembelea nyumba hiyo mwezi Januari,mwaka huu, RC Chalamila amesema,amejiridhisha kuwa kwa mujibu wa maelekezo ya mahakama nyumba hiyo ni ya Salim Selemani Salim, kwani aliinunua kisheria chini ya usimamizi wa mahakama kwa kiasi cha shilingi milioni 250 tangu mwaka 2011.
Aidha, RC Chalamila amesema, baada ya nyumba hiyo kuuzwa kisheria baadhi ya warithi walipokea fedha hizo kutoka kwa dalali wa mahakama, lakini baadhi ya warithi akiwemo Bi.Malaya waligoma kuchukua fedha hiyo ambapo kiasi cha shilingi milioni 64 na laki tano ambayo hadi sasa ipo kwa dalali huyo,hivyo ameelekeza dalali huyo kizikabidhi fedha hizo ziende mahakamani ili zikabidhiwe kwa wahusika kwa kuzingatia taratibu za kimahakama.
Akitoa taarifa ya kamati iliyoundwa na Mkuu wa Mkoa Mwenyekiti wa kamati hiyo ambaye pia ni Mwanasheria wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Fabiola Mwingira amesema, kamati imefuatilia kwa kina mgogoro huo na kubaini kuwa taratinu zote za kimahakama zilifuatwa baada ya warithi kutoelewana na mahakama kusimamia uuzwaji wa nyumba hiyo.
Kwa upande wa Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Mheshimiwa Edward Mpogolo ameshukuru mgogoro huo kumalizika na kuahidi kushirikiana na kamati yake ya usalama kuhakikisha amani inaimarika mahali hapo.





