NA LWAGA MWAMBANDE
UKIREJEA katika Biblia Takatifu kuanzia Agano la Kale na Agano Jipya utaona kuwa, neno la Mungu linaweka msimamo usiotetereka dhidi ya ushuhuda wa uongo, likisisitiza kuwa ukweli ni msingi wa haki na amani katika jamii.
Kutoka 20:16 neno linaeleza kuwa, usimshuhudie jirani yako uongo.Usiruhusu chuki ikufanye muongo, badala yake chagua heshima na ukimya kuliko uongo na dhambi.Amri hii inaonesha wazi kuwa kutoa taarifa za uongo si kosa dogo, bali ni uvunjaji wa sheria ya Mungu.
Aidha,Mithali 6:16-19 inataja shahidi wa uongo kuwa miongoni mwa mambo ambayo Bwana anayachukia, kwa sababu husababisha fitina na kuvuruga mshikamano wa kijamii.
Katika Agano Jipya, Waefeso 4:25 inawahimiza waumini kusema kweli kila mmoja na jirani yake, wakitambua kuwa ukweli hujenga umoja.
Mshairi wa kisasa Lwaga Mwambande anasisitiza kuwa, kimaadili na kijamii, ushuhuda wa uongo hudhoofisha haki, huumiza wasio na hatia na kuharibu imani katika mifumo ya sheria. Kwa mtazamo wa kibiblia, ni dhambi inayomkosea Mungu na kuidhuru jamii.
Kwa ujumla,neno la Mungu linahimiza uadilifu na ukweli kama nguzo za ustawi wa jamii, likitoa onyo kali dhidi ya mashahidi wa uongo katika nyakati zote. Endelea;
1. Mashahidi wa uongo,wapo tangia zamani,
Washabikia uongo, pesa zende mfukoni,
Hiyo yote ni michongo, hutokea duniani,
Walitokea kwa Yesu, itakuwa kwako wewe?
2. Yesu alipokamatwa, miaka ile zamani,
Ni watu waliokotwa, awekwe mashitakani,
Ushahidi kutafutwa, usokuwepo hewani,
Walitokea kwa Yesu, itakuwa kwako wewe?
3. Ni kweli tena ajabu, amini usiamini,
Walizotoa sababu, kwa uwazi bila soni,
Ndizo zilizoratibu, akatiwa hatiani,
Walitokea kwa Yesu, itakuwa kwako wewe?
4. Mwingine ndugu Nabothi, na shamba lenye thamani,
Tena lile la urithi, palipokuwa nyumbani,
Ni kweli siyo hadithi, alitiwa hatiani,
Walitokea kwa Yesu, itakuwa kwako wewe?
5. Mfalme alilitaka, alifanye bustani,
Nabothi kwa uhakika, kakataa asilani,
Ni urithi alishika, kitu kwake cha thamani,
Walitokea kwa Yesu, itakuwa kwako wewe?
6. Mbinu zikaandaliwa, za kutolewa shambani,
Mashahidi andawaliwa, ushahidi wa shetani,
Sana alifanyiziwa, akatiwa hatiani,
Walitokea kwa Yesu, itakuwa kwako wewe?
7. Yaani aliuawa, Nabothi kazikwa chini,
Na shamba likatwaliwa, litumike bustani,
Mashahidi watumiwa, ni wa uongo jamani,
Walitokea kwa Yesu, itakuwa kwako wewe?
8. Ndivyo ilivyo dunia, leo ni kama zamani,
Watu wengi wapitia, maisha yao shidani,
Wale wawafanyia, ni waongo kama nini,
Walitokea kwa Yesu, itakuwa kwako wewe?
9. Kile cha kuangalia, dhamiri yako moyoni,
Kama wapata hatia, ni kwa Mungu magotini,
Moyo utakutulia, upate amani ndani,
Walitokea kwa Yesu, itakuwa kwako wewe?
10. Mashahidi wa uongo, wakikuvaa mwilini,
Utaleta zako tungo, waweza zipiga chini,
Sababu yote mipango, ulipo upigwe chini,
Walitokea kwa Yesu, itakuwa kwako wewe ?
11. Mashahidi wa uongo, jua mko hatiani,
Hizo zenu longolongo, hazipotei angani,
Mungu yupo siyo mwongo, anawaangalieni,
Walitokea kwa Yesu, itakuwa kwako wewe?
(Mathayo 26:59-61, 1 Wafalme 21:9-13)
Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602