Serikali yafafanua hatua za kudhibiti mikopo yenye riba kubwa

CHIDAIWE MSUYA,
JORDAN MWAMBO

NAIBU Waziri wa Fedha, Mhe. Mhandisi Mshamu Ali Munde (Mb) amesema, Serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali kudhibiti mikopo yenye riba kubwa ili kulinda wananchi dhidi ya mikopo hatarishi, ikiwemo kuimarisha usimamizi wa sekta ya fedha kupitia Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Mhandisi Mshamu Ali Munde (Mb) akitoa ufafanuzi kuhusu hatua zinazochukuliwa na Serikali kudhibiti mikopo yenye riba kubwa (mikopo umiza) wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Jimbo la Kiamboni, Mhe. Nyakisa Sanga, pamoja na swali la msingi kuhusu riba za mikopo kwa wafanyakazi, bungeni jijini Dodoma.(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, WF, Dodoma).

Mhe. Munde ametoa kauli hiyo bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa Jimbo la Kigamboni, Mhe. Nyakisa Sanga, aliyetaka kufahamu hatua zinazochukuliwa na Serikali kuhakikisha wananchi, hususan wafanyakazi, hawabebeshwi mzigo wa riba kubwa za mikopo.

Ameeleza kuwa, Serikali kwa kushirikiana na BoT imeendelea kusimamia kwa karibu taasisi za fedha ili kuhakikisha zinazingatia sheria, kanuni na miongozo ya utoaji wa mikopo.

Akijibu swali la msingi lililoulizwa kuhusu wakati ambao wafanyakazi wa Tanzania watapunguziwa riba za mikopo na kufikia asilimia 7 au 8, Mhe. Munde amesema kuwa, kwa mujibu wa sera za uchumi wa nchi, riba za mikopo zinazotolewa na taasisi za fedha huamuliwa na nguvu za soko, hivyo Serikali haiwezi kuelekeza moja kwa moja taasisi hizo kuweka viwango maalum vya riba kwa kundi fulani la wakopaji.

“Riba za mikopo nchini huamuliwa na soko. Serikali ikielekeza taasisi za fedha kuweka kiwango maalum cha riba kwa wafanyakazi au mkopaji yeyote, itakuwa inakinzana na mwelekeo wa sera ya soko huria,” alisema Mhe. Munde.

Mhe. Munde alifafanua kuwa taasisi za fedha zina uhuru wa kuweka viwango vya riba vya chini ikiwemo asilimia 7 au pungufu endapo zitaona inafaa kufanya hivyo.

Aidha, wafanyakazi binafsi au kupitia waajiri wao wana fursa ya kufanya majadiliano na benki husika ili kukubaliana juu ya viwango vya riba vinavyoweza kutolewa.

Mhe. Munde alisisitiza kuwa Serikali itaendelea kuboresha mazingira ya kifedha nchini kwa lengo la kuhakikisha upatikanaji wa mikopo yenye masharti nafuu na yenye tija kwa wananchi, huku ikilinda misingi ya sera ya soko huria inayotumika nchini.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here