DAR-Naibu Waziri wa Wizara ya Uchukuzi, Mhe.David Kihenzile, ametembelea ujenzi wa ofisi za Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) zilizopo Sinza Simu 2000, jijini Dar es Salaam. Ujenzi huu, unaofadhiliwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, unalenga kuongeza ufanisi wa utoaji wa taarifa sahihi za hali ya hewa.
Akizungumza katika ziara hiyo,Naibu Waziri wa Uchukuzi, Mhe.David Kihenzile (Mb) amesema, Serikali ya Awamu ya Sita imetenga takribani shilingi bilioni 13 kwa ajili ya ujenzi wa ofisi za TMA.
Miradi hiyo inahusisha ujenzi wa jengo la kisasa la Kanda ya Mashariki na Utoaji Tahadhari za Hali ya Hewa pamoja na kituo cha tahadhari za Tsunami nchini,pamoja na Kituo cha Taifa cha Uhakiki wa Vifaa vya Hali ya Hewa (National Meteorological Calibration Centre) kitakachosaidia kukagua na kuboresha vifaa vya hali ya hewa.
Mhe. Kihenzile amesema majengo yote mawili, yaliyoanza kujengwa mwaka 2023 na 2025, yanatarajiwa kukamilika kabla ya mwisho wa mwaka huu.
Ameeleza kuwa miradi hiyo itaongeza ufanisi katika utoaji wa taarifa za hali ya hewa na kuwawezesha wataalamu kufanya kazi katika mazingira bora na ya kisasa.
Kwa niaba ya Waziri wa Uchukuzi,Mhe.David Kihenzile (MB), ametoa rai kwa Bodi na Menejimenti ya TMA kusimamia miradi hiyo kwa weledi, uzalendo na kuhakikisha inakamilika kwa wakati na kwa ubora uliokusudiwa.
Aidha aliipongeza TMA kwa kumchagua mkandarasi wa ndani, Chuo cha DIT (Taasisi ya Teknolojia ya Dar es Salaam), kutekeleza miradi hiyo akieleza kuwa hatua hiyo inachochea maendeleo ya wataalamu na taasisi za ndani.
Tags
Habari
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA)
Tanzania Meteorological Agency (TMA)
Utabiri wa Hali ya Hewa Tanzania








