Tanzania yazipongeza Ghana,Zimbabwe,Sierra Leone na APRM Afrika

ADDIS ABABA-Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imezipongeza Jamhuri za Ghana, Zimbabwe na Sierra Leone na Sekretarieti ya Mpango wa Kujitathmini kwa Hiari Afrika (APRM) kwa kukamilisha mchakato wa tathmini wa hiari chini ya utaratibu wa African Peer Review Mechanism (APRM) wa Umoja wa Afrika.
Pongezi hizo zimetolewa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thabit Kombo, kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, alipomwakilisha katika Kikao cha 35 cha Kawaida cha Jukwaa la Kujitathmini barani Afrika la Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika kilichofanyika jijini Addis Ababa, Ethiopia, pembezoni mwa Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika unaofanyika kuanzia Februari 11–15 , 2026.

Mhe. Waziri Kombo amesema, hatua iliyofikiwa na nchi hizo inaonesha dhamira ya kweli ya nchi hizo katika kuimarisha misingi ya utawala bora, uwajibikaji ili kufikia maendeleo endelevu barani Afrika.
Waziri Kombo pia amewasilisha pongezi za Tanzania kwa Sekretarieti ya APRM ya Umoja wa Afrika (AU) kwa kazi kubwa na ya kitaalamu inayoendelea kufanya katika kuratibu tathmini hizo pamoja na kusimamia utekelezaji wa mapendekezo yanayotolewa na nchi wanachama.
"Sekretarieti ya APRM ya AU imeendelea kuwa chombo muhimu katika kuhamasisha uwazi, uwajibikaji na kubadilishana uzoefu miongoni mwa nchi wanachama, Tanzania inaipongeza sana Sekretarieti,” alisema Waziri Kombo.

Waziri Kombo aliahidi kuwa Tanzania itaendelea kushirikiana kikamilifu na Sekretarieti ya APRM pamoja na nchi nyingine za Afrika katika kutekeleza na kufanikisha malengo ya chombo hicho na kusisitiza kuwa kupitia mshikamano na ushirikiano wa dhati, mataifa ya Afrika yataweza kuimarisha taasisi zake, kukuza demokrasia na kuhakikisha kunakuwepo na maendeleo jumuishi kwa manufaa ya wananchi wake.
Kikao hicho cha ngazi ya juu kiliandaliwa chini ya Mpango wa Kujitathmini kwa Hiari Barani Afrika wa Umoja wa Afrika (AU) uliwakutanisha viongozi wa Afrika kwa lengo la kupitia maendeleo ya utawala bora, kubadilishana uzoefu na kuimarisha mifumo ya uwajibikaji barani Afrika.
Mkutano huo ulihudhuriwa na Marais kutoka nchi za Angola, Burundi, Namibia, Msumbiji, Zimbabwe, Makamu wa Rais wa Kwanza wa Uganda na Mawaziri wa Mambo ya Nje ambao waliwawakilisha Wakuu wa Nchi nyingine za Afrika.Katika Kikao hicho Jamhuri ya Uganda ilichukua uenyekiti wa APRM kwa kipindi cha Miaka miwili kutoka kwa Jamhuri ya Angola ambayo imemaliza muda wake

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here