PWANI-Jeshi la Polisi Kikosi cha Reli Tanzania limetoa elimu ya Usalama wa miundombinu ya Shirika la Reli Tanzania kwa wafugaji wanaoishi na kufanya shughuli zao pembezoni kwa njia ya reli.
Elimu hiyo imetolewa na Kamanda wa Polisi Kikosi cha Reli Tanzania, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Matride Kuyeto akiambatana na Afisa Polisi Jamii wa Kikosi hicho Kamishna Msaidizi wa Polisi ACP Batiseba Kasanga, Februari 21, 2026 katika mnada wa wafugaji kata ya Kwala, Wilaya ya Kibaha, Mkoa wa Pwani.
Akizungumza na wafugaji hao wanaoishi pembezoni mwa ushoroba wa reli, Kamanda Matride Kuyeto amewataka kutoingiza mifugo yao katika sehemu zisizo ruhusiwa ili kuepusha kuleta athari kwa binadamu wanaotumia treni kama chombo cha usafiri na kuhatarisha usalama wa miundombinu ya reli.
Aidha, ACP Kuyeto ametoa rai kwa wafugaji hao kwa kila mmoja atimize wajibu wake kwa kudhibiti mifugo yake ili kuzuia madhara katika njia ya reli, pia amewataka waendelee kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu kwa lengo la kuendelea kudhibiti vitendo vya kihalifu.
Naye, ACP Batiseba Kasanga ameongea na wafugaji hao na kuwataka wazingatie elimu wanayoipata na kuifikisha kwa watoto wao ambao kwa kiasi kikubwa ndio wachungaji wa mifugo yao.
“Waelekezeni watoto wenu kwamba kufanya shughuli za uchungaji karibu na njia ya reli ni kosa pia ni hatari kwao pamoja na mifugo,”amesema ACP Batiseba.




