DODOMA-Wakulima Chemba mkoani Dodoma watakiwa kujisajili katika mfumo rasmi wa pembejeo za ruzuku ili kunufaika na ruzuku inayotolewa na serikali kwa wakulima.
Hayo yamebainishwa Februari 16,2026 na Meneja wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania Kanda ya Kati,Levocatus Rwegoshora, wakati wa kampeni ya Mali shambani iliyolenga kuhamasisha wakulima kujisajili katika mfumo rasmi wa ruzuku ili waweze kupata pembejeo za kilimo kwa bei ya nafuu.Amesema kuwa, usajili huo unawawezesha wakulima kunufaika moja kwa moja na Mpango wa ruzuku za pembejeo za killmo wa Serikali na kuwafanya kuongeza tija ya uzalishaji wa mazao ya kilimo.
Kwa upande wake Mtafiti na Mkaguzi wa Ubora wa Mbegu kutoka Taasisi ya Kuthibiti Ubora wa Mbegu Tanzania (TOSCI), Dkt. Neema Yohana, amesema Serikali imetoa ruzuku ya pembejeo muhimu za kilimo ikiwemo mbegu, mbolea na viuatilifu, na kusisitiza kuwa wakulima wanapaswa kununua pembejeo kupitia mfumo rasmi ili kupata bidhaa zilizoidhinishwa na zenye ubora.
Aliongeza kuwa, wakulima wanaweza kuthibitisha ubora wa mbegu kwa kutumia vocha zinazopatikana kwenye kifungashio cha mbegu kwa kupiga *148*52 # kufuata maelekezo kisha ingiza namba ya vocha ili kujiridhisha kama mbegu ni halisi na imethibitishwa.
Naye mkulima kutoka Kijiji cha Paranga. Ramadhani Sunuku, aliwashukuru wataalam kwa kuwafikia na kuwapatia elimu, akisema mafunzo hayo yamemhamasisha kujisajili kwenye mpango wa ruzuku pamoja na kutumia mbolea kwa usahihi, jambo analotarajia kuongeza uzalishaji wake kutoka magunia matatu hadi kufikia magunia ishirini na tano kwa ekari.
Kampeni ya Mali Shambani inalenga kuongeza uelewa kwa wakulima kuhusu matumizi sahihi ya pembejeo za kilimo na umuhimu wa kupima afya ya udongo na kujisajili katika mpango wa ruzuku pembejeo za kilimo , hatua inayotarajiwa kuchochea uzalishaji wenye tija na kuimarisha usalama wa chakula nchini.






























