ADDIS ABABA-Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thabit Kombo (Mb), ametoa wito wa kuimarishwa kwa ushirikiano miongoni mwa nchi wanachama wa Bonde la Mto Nile.
Balozi Kombo ametoa wito huo katika Kikao cha Ngazi ya Juu cha Bonde la Mto Nile kilichofanyika pembezoni mwa Mkutano Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika unaoendelea jijini Addis Ababa, Ethiopia February 11-15, 2026.
Kupitia kikao hicho Mheshimiwa Waziri Kombo alithibitisha dhamira ya Tanzania ya kuendelea kuimarisha ushirikiano, mazungumzo na usimamizi endelevu wa rasilimali maji ya Mto Nile kwa manufaa ya nchi zote zinazozunguka bonde hilo.
Akizungumza mbele ya Mawaziri na wawakilishi kutoka nchi za Bonde la Nile, Waziri Kombo amesisitiza umuhimu wa kuimarisha mifumo ya taasisi za bonde hilo na kusisitiza kuwa, uimarishaji wa mifumo hiyo utatoa mfumo wa kudumu utakaoratibiwa vizuri na hivyo kuimarisha ushirikiano na kuhakikisha matumizi ya haki na yenye uwiano ya rasilimali maji ya pamoja.
“Tunaikaribisha na kuiunga mkono kikamilifu kuanzishwa kwa Tume ya Bonde la Mto Nile,” alisema Waziri Kombo na kuongeza,“Muhimu zaidi, tunaunga mkono juhudi zinazoendelea za kuzijumuisha nchi zote zinazohusika na kupitia mazungumzo ya kujenga na uelewano wa pamoja, tutaweza kutatua tofauti zetu.”
Waziri Kombo alieleza kuwa Tanzania inaunga mkono utekelezaji wa Mpango wa Uwekezaji wa Bonde la Mto Nile unaojumuisha miradi ya kimkakati inayolenga kuimarisha usalama wa maji, nishati, uzalishaji wa chakula na uhifadhi wa mazingira katika ukanda wa Bonde la Nile.
Alibainisha kuwa, uwekezaji wa pamoja katika miundombinu, ustahimilivu dhidi ya mabadiliko ya tabianchi na miradi ya nishati jadidifu utapunguza athari za changamoto zilizopo na kufungua fursa za ustawi wa pamoja kwa nchi wanachama.
Amezisihi nchi husika kuendelea na mazungumzo na kuepuka hatua zinazoweza kuongeza mvutano na kusisitiza kuwa Tanzania itaendelea kuhimiza mazungumzo ya amani, kuheshimiana na kutafuta suluhisho za changamoto kwa misingi ya Kiafrika ili kulifanya Bonde la Nile kuwa mfano wa umoja na maendeleo endelevu barani Afrika.
Mkutano huo uliandaliwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Ethiopia, Mheshimiwa Gedion Timotheos na kuhudhuriwa na Mawaziri wa Mambo ya Nje kutoka nchi za Bonde la Nile ambazo ni Burundi, Rwanda, Kenya, Uganda, Ethiopia na Sudani kusini.









