DODOMA-Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), amewashukuru Wabunge na wajumbe wa Kamati ya Mipango kwa maoni na ushauri waliotoa kwa ajili ya kuboresha Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2026/27-2028/29.
Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), alitoa shukurani hizo wakati akihitimisha mjadala wa Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali katika kipindi cha muda wa kati kwa mwaka 2026/2027 hadi 2028/2029, bungeni, jijini Dodoma.
Mhe.Balozi Omar alisema sehemu kubwa ya michango ya Wabunge ilielekezwa katika maeneo ya ukusanyaji wa mapato ya ndani, fursa za ukopaji kwa Serikali, mwenendo wa utekelezaji wa miradi ya maendeleo, utekelezaji wa sera ya fedha na maboresho ya maelekezo yaliyoainishwa katika Mwongozo.
Alisema katika wasilisho hilo alilowasilisha 02 Februari, 2026 alieleza mambo mbalimbali ikiwemo mwenendo na mwelekeo wa hali ya uchumi na utekelezaji wa bajeti ya Serikali kwa mwaka 2024/25, vipaumbele vya mpango na bajeti ya Serikali kwa mwaka 2026/27 – 2028/29, na maelekezo muhimu ya kuzingatiwa na maafisa masuuli wakati wa kuandaa, kutekeleza, kufuatilia, kutathmini na kutoa taarifa za utekelezaji wa bajeti.
Aliongeza kuwa, mwongozo huo unaakisi juhudi za Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuboresha maisha ya Watanzania kwa kuendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji na biashara ili kuvutia uwekezaji wa sekta binafsi, kuimarisha upatikanaji wa huduma za jamii, kuweka msukumo katika kuimarisha sekta za uzalishaji, na kudumisha amani, usalama, utawala bora na utawala wa sheria, umoja na utulivu nchini.
Aidha, aliwashukuru na kuwapongeza wafanyabiashara na wawekezaji kwa mchango wao katika ulipaji wa kodi, uzalishaji wa ajira, ushiriki katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kutoa huduma za kijamii kwa wananchi, na kuwashukuru wananchi kwa mwitikio wa kulipa kodi kwa hiari.
