BoT yazidi kuwapambania wanawake katika uongozi

NA GODFREY NNKO

GAVANA wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Bw.Emmanuel Tutuba amesisitiza umuhimu wa benki na taasisi za kifedha nchini kuimarisha usawa wa kijinsia katika ngazi za juu za uongozi, akieleza kuwa hatua hiyo ni muhimu katika kukuza uchumi jumuishi na maendeleo endelevu.
Ameyasema hayo leo Machi 30,2026 katika makao makuu ndogo ya BoT jijini Dar es Salaam wakati akifungua Mkutano wa Pili wa Mabenki na Viongozi wa Taasisi za Kifedha Nchini kwa mwaka 2026.

Akizungumza katika mkutano huo ambao pia ni kilele cha maadhimisho maalum ya Siku ya Wanawake yaliyowakutanisha watendaji wakuu wa benki zote nchini, pamoja na wawakilishi wa taasisi za kifedha na mashirika ya kimataifa yanayounga mkono sekta hiyo, Gavana Tutuba amesema, mkutano huo unajadili mafanikio mbalimbali yaliyopatikana katika sekta ya fedha nchini.

Amefafanua kuwa,mwaka uliopita alitoa waraka rasmi kwa mabenki yote nchini akiyataka kuhakikisha kuwa ifikapo Juni,2028 wanawake wanapata uwiano wa angalau asilimia 30 katika bodi za wakurugenzi na menejimenti za taasisi hizo.

“Ninashukuru kuona kuwa tayari benki 22 kati ya benki 42 zimefikia lengo la kuwa na angalau asilimia 30 ya wanawake katika bodi na menejimenti zao,” amesema Gavana Tutuba.

Hata hivyo, amezitaka benki ambazo bado hazijafikia kiwango hicho kuongeza juhudi, akibainisha kuwa changamoto zilizopo zinahusiana na taratibu za upatikanaji wa wajumbe wa bodi pamoja na wataalamu wenye sifa stahiki, hususan wanawake.

Gavana huyo ameongeza kuwa,ataendelea kufuatilia utekelezaji wa waraka huo hadi kufikia muda uliopangwa wa Juni,2028 huku akizipongeza taasisi zilizofanikiwa na kuzihimiza zile zilizo katika hatua za utekelezaji kuongeza kasi.

Aidha, amesisitiza umuhimu wa benki kuweka mikakati madhubuti ya kuwawezesha wanawake kiuchumi kwa kuwapatia fursa mbalimbali, ikiwemo huduma za kifedha, elimu na ushiriki katika shughuli za maendeleo.

Kwa mujibu wa Gavana Tutuba, jitihada zinazoendelea zimeanza kuzaa matunda, ambapo mafanikio makubwa yanaonekana kutokana na mikakati inayotekelezwa na taasisi za kifedha nchini.

Pia, amesisitizwa kuwa,matumizi ya takwimu sahihi na zilizochambuliwa kwa kuzingatia vigezo kama jinsia, umri, eneo na aina ya shughuli za kiuchumi ni muhimu katika kuhakikisha sera na programu zinakuwa na tija na kuwafikia walengwa kwa ufanisi.
Kwa upande wa ushirikiano, Gavana Tutuba amezitaka taasisi za kifedha kuimarisha juhudi za pamoja katika maeneo ya elimu ya fedha, utafiti na upanuzi wa huduma vijijini, ambako kiwango cha ujumuishwaji wa kifedha bado ni cha chini katika baadhi ya mikoa.

Vilevile, Gavana Tutuba ametoa rai kwa Umoja wa Mabenki Tanzania (TBA kuratibu programu za elimu ya fedha zinazowalenga wanawake na kutoa taarifa za utekelezaji wake kwa Benki Kuu kila robo mwaka.

Pia, umoja huo umeshauriwa kuongoza juhudi za pamoja za kuongeza upatikanaji wa huduma za kifedha katika maeneo yenye uhitaji mkubwa.

Kupitia programu za elimu ya fedha zinazoendeshwa na Chuo cha Benki Kuu (BoT Academy), zaidi ya Watanzania milioni 1.6 tayari wamefikiwa, huku mitaala ya elimu ya fedha ikiingizwa rasmi katika mfumo wa elimu nchini kuanzia ngazi ya msingi hadi vyuo vikuu.

BoT pia imebainisha mipango ya kuanzisha mifumo ya kusaidia upatikanaji wa mikopo kwa wajasiriamali, hasa wanawake ambao hukabiliwa na changamoto za ukosefu wa dhamana, historia ya mikopo na faida zinazoonekana katika biashara zao.

Amesema kuwa, wanawake wanaojihusisha na biashara ndogo na za kati ni fursa kubwa ambayo bado haijatumika kikamilifu katika kukuza uchumi.

Hivyo, kuongeza upatikanaji wa huduma za kifedha na kuondoa vikwazo vya kimuundo kutachangia kwa kiasi kikubwa kufikia malengo ya Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050.

Gavana Tutuba ameongeza kuwa, Benki Kuu itaendelea kuunga mkono juhudi zote zinazolenga kujenga sekta ya fedha iliyo jumuishi, imara na endelevu, huku akieleza imani kuwa jukwaa hilo litaimarisha ushirikiano na kuongeza ufanisi wa juhudi za pamoja katika sekta hiyo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here