TABORA-Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Tabora, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi,SACP Richard Abwao, amefika katika Shule ya Sekondari Kaliua iliyopo Wilaya ya Kaliua mkoani Tabora kufuatia tukio la moto lililotokea katika bweni la wasichana Machi 23, 2026.
Kwa mujibu wa taarifa za awali, moto huo ulizuka ndani ya bweni moja la wanafunzi wa kike na kusababisha uharibifu wa miundombinu pamoja na mali mbalimbali za wanafunzi.Hata hivyo, imethibitishwa kuwa hakuna madhara yoyote ya kibinadamu yaliyoripotiwa katika tukio hilo.
Mali zilizoteketea ni pamoja na magodoro, nguo, vitabu na daftari za wanafunzi, hali iliyosababisha hasara kubwa kwa wahusika.Akizungumza baada ya kutembelea eneo la tukio, SACP Abwao alitoa pole kwa uongozi wa shule, wanafunzi na wazazi kwa tukio hilo, huku akisisitiza kuwa uchunguzi unaendelea ili kubaini chanzo cha moto huo.
Aidha, alieleza kuwa tathmini ya kina inaendelea kufanyika ili kubaini thamani ya mali zilizoharibiwa na moto huo, huku akiahidi kuwa hatua stahiki zitachukuliwa mara baada ya kukamilika kwa uchunguzi.

