Dar yatoa fungu kujenga vituo vya afya, ofisi za mitaa na kituo cha polisi

NA DIRAMAKINI

HALMASHAURI ya Jiji la Dar es Salaam imetenga jumla ya Shilingi 451,663,080 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo ujenzi na ukamilishaji wa ofisi za mitaa, vituo vya afya, zahanati pamoja na kituo cha polisi, kwa lengo la kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.
Kwa mujibu wa taarifa kwa umma iliyotolewa na Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, Elihuruma Mabelya imeeleza kuwa, fedha hizo zimeelekezwa katika miradi sita muhimu inayolenga kuimarisha miundombinu ya huduma za kijamii na kiutawala katika maeneo mbalimbali ya jiji.

Aidha, kwa mujibu wa taarifa hiyo, kati ya miradi itakayotekelezwa ni ujenzi wa Kituo cha Polisi katika Kata ya Bonyokwa utakaogharimu Shilingi milioni 150, huku Shilingi 111,663,080 zikitumika kukamilisha ujenzi wa Kituo cha Afya Mvuti kilichopo Kata ya Msongola.

Pia, fedha hizo zitatumika kukamilisha ujenzi wa Ofisi ya Mtaa wa Kichangani katika Kata ya Chanika, Ofisi ya Mtaa wa Viwege katika Kata ya Majohe pamoja na Ofisi ya Mtaa wa Mnyamani katika Kata ya Mnyamani, ambapo kila mradi umetengewa Shilingi milioni 30.

Vilevile, Shilingi milioni 100 zimetengwa kwa ajili ya ukarabati wa Zahanati ya Kitunda iliyopo katika Kata ya Kitunda.

Mabelya amesema,utekelezaji wa miradi hiyo unalenga kuboresha mazingira ya kazi kwa watumishi wa umma pamoja na kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma kwa wananchi wa Jiji la Dar es Salaam.

Ametoa wito kwa wakazi wa kata na mitaa husika kushirikiana na viongozi pamoja na kamati za usimamizi wa miradi ili kuhakikisha utekelezaji wake unafanyika kwa wakati na kwa kuzingatia viwango vilivyowekwa.

“Viongozi na kamati husika wanapaswa kusimamia ipasavyo matumizi ya fedha za umma ili kuhakikisha thamani halisi ya fedha inapatikana katika utekelezaji wa miradi hii."

Amesisitiza kuwa, usimamizi madhubuti wa miradi hiyo utasaidia kufanikisha lengo la serikali la kuboresha huduma za kijamii na kuimarisha maendeleo ya wananchi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here