NA GODFREY NNKO
GAVANA wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT),Bw. Emmanuel Tutuba ametoa wito kwa Watanzania kuendelea kuliombea Taifa amani, upendo na mshikamano ili kudumisha utulivu wa kijamii na kiuchumi katika kipindi ambacho uchumi wa dunia unakabiliwa na changamoto mbalimbali.

Akizungumza Machi 6, 2026 katika hafla ya futari iliyoandaliwa na Benki Kuu ya Tanzania katika makao makuu ndogo ya benki hiyo jijini Dar es Salaam, Gavana Tutuba alisema ni muhimu kwa wananchi kuendeleza uzalendo na ushirikiano katika kujenga uchumi wa nchi.Alisema, dunia kwa sasa inakabiliwa na changamoto kadhaa zikiwemo vita, mivutano ya kisiasa katika baadhi ya mataifa, mabadiliko ya tabianchi pamoja na misukosuko mingine ya kiuchumi inayojitokeza katika masoko ya kimataifa.
"Ni muhimu tuendelee kuliombea taifa letu amani, upendo na mshikamano. Pia tuendelee kudumisha uzalendo na ushirikiano katika kujenga uchumi wetu,” alisema Tutuba katika hafla hiyo iliyowakutanisha viongozi wa dini, wadau wa sekta ya fedha pamoja na wananchi mbalimbali wa Mkoa wa Dar es Salaam.
Katika hotuba yake, Gavana Tutuba alisisitiza kuwa Benki Kuu inatambua na kuthamini mchango wa taasisi za dini katika kuimarisha maadili mema kwa waumini wake.
Alisema, maadili hayo ni msingi muhimu katika kujenga jamii yenye uwajibikaji na watumishi waadilifu katika taasisi mbalimbali za umma na binafsi nchini.
Aidha, alikumbusha kuwa Benki Kuu ya Tanzania ilianzishwa rasmi Juni 14, 1966 na kwamba mwaka huu taasisi hiyo itatimiza miaka 60 tangu kuanzishwa kwake.Kwa mujibu wa Gavana Tutuba, miaka 60 ni kipindi muhimu kinachoonesha ukomavu wa taasisi hiyo katika kutekeleza majukumu yake ya msingi kwa ustadi na ufanisi.
“Wapo wanaosema miaka 60 ni umri wa kustaafu, lakini pia ni umri wa ukomavu wa kimawazo, kiakili na kiutendaji. Tunaamini katika kipindi hiki Benki Kuu imefanikiwa kujenga heshima na kufanya vizuri kwa viwango vya kimataifa,” alisema.
Alieleza kuwa, katika kipindi hicho, benki imeendelea kusimamia kwa karibu ukuaji wa uchumi wa taifa, kudhibiti mfumuko wa bei, kulinda thamani ya shilingi pamoja na kusimamia urari wa malipo ya nchi.
Kadhalika, alisema BoT imeendelea kuchapisha na kusambaza fedha kulingana na mahitaji ya uchumi wa taifa, pamoja na kusimamia mifumo ya malipo kwa kutumia teknolojia za kisasa ili kuhakikisha huduma za kifedha zinafika kwa wananchi kwa ufanisi.
Kuhusu hatua ya benki kuu kununua na wakati mwingine kuuza dhahabu, Gavama Tutuba alieleza kuwa, hatua hiyo ni utekelezaji wa matakwa ya sheria pamoja na mkakati wa usimamizi wa akiba ya fedha za kigeni ya taifa.
Alifafanua kuwa, kwa mujibu wa Sheria ya Benki Kuu, kifungu cha tano kinaelekeza benki kununua dhahabu kama sehemu ya kuhifadhi akiba ya fedha za kigeni kwa ajili ya kulinda mustakabali wa uchumi wa nchi.
Aidha, alisema kifungu cha 52 cha sheria hiyo kinairuhusu benki kufanya shughuli mbalimbali kuhusiana na mali za akiba ya fedha za kigeni, ikiwemo kununua, kuuza, kuwekeza au kuagiza mali hizo kulingana na mahitaji ya usimamizi wa akiba ya taifa.
Gavana Tutuba alibainisha kuwa,maamuzi ya kununua au kuuza dhahabu hutegemea mwenendo wa bei katika soko la dunia.
Alisema, inapojitokeza hali ya bei ya dhahabu kupanda kwa kiwango kikubwa katika masoko ya kimataifa, benki inaweza kuuza sehemu ya akiba hiyo ili kupata fedha za kigeni, hasa dola za Marekani, na baadaye kununua tena dhahabu endapo bei itashuka.
Aliongeza kuwa,hatua hiyo ni sehemu ya usimamizi wa hatari zinazotokana na mabadiliko ya bei katika masoko ya fedha duniani, akibainisha kuwa soko la dhahabu lina tabia ya kubadilika kwa kasi, hivyo maamuzi hayo hufanywa kwa misingi ya kitaalamu kama ilivyo katika biashara na uwekezaji wa masoko ya fedha.
Gavana Tutuba pia alikiri kuwa baadhi ya wananchi wasiokuwa na uelewa wa kina kuhusu masoko ya fedha wanaweza kuwa na maswali kuhusu hatua hizo, lakini alisisitiza kuwa benki inaendelea kutoa elimu kwa umma ili kuongeza uelewa na kuwahamasisha wananchi kushiriki katika uwekezaji na shughuli za masoko ya fedha nchini.
Wakati huo huo, Gavana Tutuba alisema, mifumo ya malipo nchini imeendelea kufanya kazi kwa ufanisi katika maeneo ya mijini na vijijini, hali inayochangia kuimarisha shughuli za kiuchumi kwa wananchi na taasisi mbalimbali nchini. Soma hapa, Sera imara za kiuchumi zachochea ukuaji wa uchumi wa Tanzania

























