Kuharibu mazingira,twajimaliza wenyewe

NA LWAGA MWAMBANDE

UHARIBIFU wa mazingira ni tatizo kubwa linaloathiri dunia katika nyanja mbalimbali za maisha ya binadamu.
Shughuli kama ukataji ovyo wa misitu, uchafuzi wa hewa na maji, pamoja na matumizi mabaya ya ardhi zimechangia kwa kiasi kikubwa kuongezeka kwa tatizo hili.

Mosi,uharibifu wa mazingira husababisha kuongezeka kwa magonjwa kwa binadamu kutokana na uchafuzi wa hewa na maji.

Maji yasiyo safi na hewa yenye sumu huweza kusababisha magonjwa ya kuambukiza na ya mfumo wa upumuaji, hivyo kuhatarisha afya za wananchi.

Pili, huathiri uzalishaji wa chakula kwa kusababisha mmomonyoko wa udongo na kupungua kwa rutuba ya ardhi. Hali hii husababisha kupungua kwa mavuno na kuongeza hatari ya uhaba wa chakula katika jamii.

Aidha, uharibifu wa mazingira husababisha kupotea kwa viumbe hai na kuathiri mizania ya asili ya mazingira.

Ili kukabiliana na changamoto hii, ni muhimu kwa jamii na Serikali kushirikiana katika kulinda mazingira kwa kupanda miti, kutumia rasilimali kwa uangalifu na kuzingatia sheria za uhifadhi wa mazingira.

Kwa ujumla, uhifadhi wa mazingira ni jukumu la kila mtu ili kuhakikisha maendeleo endelevu na maisha bora kwa vizazi vya sasa na vijavyo, kwani kuharibu mazingira tunajimaliza wenyewe. Endelea;

1. Ukitunza mazingira, mwenyewe unajitunza,
Yaharibu mazingira, mwenyewe unajiponza,
Ukiwa nayo busara, yatunze yatakutunza,
Kuharibu mazingira, twajimaliza wenyewe.

2. Unazo nyingi bidhaa, kutumia unaweza,
Mahali hapo wakaa, mabaki watelekeza,
Jua waleta balaa, ambalo takuumiza,
Kuharibu mazingira, twajimaliza wenyewe.

3. Pengine wakunywa maji, kiu weze maliza,
Na kisha chupa ya maji, waacha unaipuza,
Uchafuzi si mtaji, mwenyewe wajimaliza,
Kuharibu mazingira, twajimaliza wenyewe.

4. Uchafu unazagaa, kutupa umemaliza,
Mwingine kule kakaa, mazingira ayapuza,
Huo wako ukichaa, mwishowe watumaliza,
Kuharibu mazingira, twajimaliza wenyewe.

5. Kuzitupa taka hovyo, mahali unazijaza,
Dunia jinsi ilivyo, athari zinateleza,
Hapatabaki palivyo, mwenyewe wajiunguza,
Kuharibu mazingira, twajimaliza wenyewe.

6. Pengine ni mifereji, ile maji yachuruza,
Tena hayapiti maji, taka zimeshaijaza,
Mvua kunyesha maji, njenje yabakiza,
Kuharibu mazingira, twajimaliza wenyewe.

7. Mafuriko yanakuja, maisha yanapoteza,
Na mali moja kwa moja, hasara umechagiza,
Ni la kwako tendo moja, mazingira kutotunza,
Kuharibu mazingira, twajimaliza wenyewe.

8. Miti kuikatakata, uasili kupoteza,
Maporomoko twapata, ardhi inatumeza,
Twatapatapa kupita, ndivyo tunajimaliza,
Kuharibu mazingira, twajimaliza wenyewe.

9. Ona sasa mafuriko, mjini yajieneza,
Na mifereji iliko, taka tumeshazijaza,
Vema tupate mwamko, maisha kuyageuza,
Kuharibu mazingira, twajimaliza wenyewe.

10. Umeshika takataka, jua wapi wazitunza,
Wala siyo kuachika, popote unapoweza,
Huko ni kuwajibika, tena huko kujitunza,
Kuharibu mazingira, twajimaliza wenyewe.

11. Tumeshaona athari, zile zatumaliza,
Kwetu ni shari na hari, hali inatuunguza,
Iwe yetu tahadhari, ubaya kuukatiza,
Kuharibu mazingira, twajimaliza wenyewe.

12. Kama tukibadilika, mazingira tukatunza,
Vile tuliathirika, na jinsi tumejifunza,
Hali itabadilika, vizuri tutajitunza,
Kuharibu mazingira, twajimaliza wenyewe.

13. Tukitunza mazingira, vyote vile tunaweza,
Sisi ni maisha bora, kwetu tutayaeneza,
Hata kesho si hasara, tena watatupongeza,
Kuharibu mazingira, twajimaliza wenyewe.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here