ZANZIBAR-Mke wa Rais wa Zanzibar, Msarifu na Mwenyekiti wa Zanzibar Maisha Bora Foundation, Mhe.Mama Mariam Mwinyi ametoa mkono wa Eid kwa wazee na watoto yatima, sambamba na kuwatakia heri na baraka za Sikukuu ya Eid el-Fitr.
Mkono huo wa Eid umetolewa Machi 21,2026 wakati Mama Mariam Mwinyi alipofanya ziara katika vituo vya kulelea wazee na watoto yatima vya Mazizini, Fuoni Mambosasa pamoja na Makaazi ya Wazee Sebleni na Welezo.
Akizungumza katika ziara hiyo,Mama Mariam Mwinyi amesema,Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kuwajali wazee wasiojiweza na mayatima kwa kuhakikisha wanapata matunzo bora, huduma stahiki pamoja na mazingira salama kwa ustawi wao.
Ameeleza kuwa, utaratibu wa utoaji wa mkono wa Eid unalenga kuwafariji, kuwaweka karibu na jamii na kuwafanya wajione kuthaminiwa, sambamba na kuwawezesha kusherehekea sikukuu kwa furaha na amani.
Aidha, Mhe.Mama Mariam Mwinyi amewanasihi waumini wa dini ya Kiislamu pamoja na wananchi kwa ujumla kuendelea kushikamana katika ibada na kutenda mema yanayompendeza Mwenyezi Mungu, hususan katika kipindi hiki cha sikukuu.
Vilevile, amewataka wazee na walezi kuwa makini na watoto ili kuepusha ajali za barabarani pamoja na vitendo vya ukatili dhidi ya watoto.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe. Zawadi Hemed Nassor, amemshukuru Mama Mariam Mwinyi kwa kuonesha upendo na utu kwa makundi maalum, pamoja na kuendeleza utaratibu wa kuwafikia na kuwafariji katika maeneo yao.
Tags
Dkt.Hussein Ali Mwinyi
Habari
Mama Mariam Mwinyi
Zanzibar Maisha Bora Foundation (ZMBF)
Zanzibar News



















