Mhasibu Msaidizi wa Zahanati ya Gidas hatiani kwa kosa la kughushi

MANYARA-Mahakama ya Wilaya ya Babati mkoani Manyara imemtia hatiani aliyekuwa Mhasibu Msaidizi wa Zahanati ya Gidas, Bw. Mohamed Twalib Baya kwa kosa la kughushi nyaraka na kujipatia fedha kinyume cha sheria.
Hukumu hiyo ilitolewa Machi 5,2026 katika shauri la Jinai Na. 2979/2026, ambapo mshtakiwa alipatikana na hatia ya kughushi kinyume na vifungu vya 333, 335(a) na 337 vya Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16 marejeo ya mwaka 2023.

Kwa mujibu wa ushahidi uliowasilishwa mahakamani, mshtakiwa alighushi sahihi za watia saini wa akaunti ya Zahanati ya Gidas na kisha kutoa fedha kutoka katika akaunti hiyo bila idhini. Kupitia udanganyifu huo, alichukua jumla ya shilingi milioni 5,426,000 ambazo alizifanyia ubadhirifu.

Akisoma hukumu hiyo, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Babati, Mhe. Victor Kimario, alimkuta mshtakiwa na hatia baada ya kufanyika kwa makubaliano ya kukiri kosa (plea bargaining) kati ya mshtakiwa na Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP).

Kutokana na makubaliano hayo, mahakama ilimhukumu mshtakiwa kifungo baridi cha miezi mitatu pamoja na amri ya kurejesha fedha zote alizozifanyia ubadhirifu kiasi cha shilingi 5,426,000 kwa mhanga.

Ilielezwa mahakamani kuwa, hadi wakati hukumu inasomwa, mshtakiwa alikuwa tayari amerejesha fedha zote hizo kwa kuweka kiasi hicho katika akaunti ya Zahanati ya Gidas iliyopo katika Benki ya NMB.

Shauri hilo liliendeshwa na waendesha mashtaka kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Manyara, ambao ni Neema Gembe, Davis Masambu na Catherine Ngessy.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here