Mwinjilisti Temba aibua hoja mpya Barabara ya Morogoro,atoa mapendekezo muhimu

DAR-Mwinjilisti wa Kimataifa, Dkt.Alphonce Temba ametoa wito kwa Serikali kuchukua hatua za haraka za kujenga upya au kupanua Barabara ya Morogoro kufuatia kuharibika kwa baadhi ya makaravati na kusababisha ajali ikiwemo eneo la Ruvu Darajani.
Akizungumza jijini Dar es Salaam leo Machi 14, 2026, Dkt.Temba amesema,miundombinu ya makaravati katika barabara hiyo imechakaa kutokana na umri mkubwa wa matumizi pamoja na kuongezeka kwa uzito na wingi wa magari yanayopita kila siku.

Kwa mujibu wa maelezo yake, Machi 13, 2026 magari sita yalianguka katika eneo la Ruvu Darajani kutokana na kuchoka kwa miundombinu ikiwemo kuharibika kwa kalavati kutokana na matumizi ya muda mrefu.

Ajali hiyo imetokea eneo lililokuwa linajengwa kiwanda cha Nyama Ruvu Darajani kilichokufa na mita miatatu karibu na daraja la Reli toka Dar es Salaam kwenda Tanga na Kilimanjaro. 

Amesema,tukio hilo linaonesha wazi umuhimu wa kufanya tathmini ya haraka ya miundombinu ya barabara hiyo ili kuepusha ajali zaidi na hasara kwa wananchi na wafanyabiashara wanaotumia njia hiyo muhimu ya usafiri.

Dkt.Temba amewataka viongozi wa Serikali, akiwemo Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, pamoja na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji,Profesa Kitila Mkumbo kushirikiana ili kuhakikisha kunapatikana suluhisho la kudumu kwa changamoto ya miundombinu ya Barabara ya Morogoro.

Amesema,Waziri wa Mipango na Uwekezaji ana jukumu muhimu katika kuhakikisha mradi wa ujenzi au upanuzi wa barabara hiyo unaingizwa katika mipango mikubwa ya maendeleo ya taifa ili kupata rasilimali zinazohitajika kwa utekelezaji wake.

“Tunatambua kuwa mipango ya maendeleo ya taifa inaongozwa na sera na mikakati ya uwekezaji. Hivyo, ni muhimu kwa Wizara ya Mipango kuhakikisha barabara hii inawekwa katika vipaumbele vya kitaifa ili kupata fedha za kutosha kwa ajili ya ujenzi wake,” amesema.
Dkt.Temba amependekeza kwa Serikali kuanzisha mradi mkubwa wa kupanua au kujenga upya Barabara ya Morogoro kuanzia Kibaha hadi Morogoro, mradi ambao anaeleza unaweza kugharimu takribani shilingi trilioni mbili.

Amesema,moja ya njia zinazoweza kutumika kupata fedha hizo ni kuongeza tozo ndogo katika baadhi ya bidhaa au huduma ili kuimarisha mfuko wa maendeleo ya miundombinu.

Kwa mujibu wake, uwekezaji huo utakuwa na manufaa makubwa kwa uchumi wa taifa kutokana na umuhimu wa barabara hiyo katika usafirishaji wa mizigo na abiria ndani na nje ya nchi.

Aidha, Dkt.Temba amependekeza kuitishwa kwa kikao cha dharura cha Bunge ili kujadili changamoto za miundombinu ya barabara hiyo na kufikia makubaliano ya haraka juu ya utekelezaji wa mradi wa uboreshaji wake.

Amesema,ucheleweshaji wa maamuzi unaweza kuendelea kusababisha hasara kubwa za kiuchumi pamoja na hatari za ajali kwa watumiaji wa barabara hiyo.

Kwa mujibu wa takwimu zilizoripotiwa na BBC News mwaka 2024, Barabara ya Morogoro inapokea takribani magari 340,000 ndani ya saa 24, hali inayoifanya kuwa miongoni mwa barabara zenye msongamano mkubwa nchini.

Barabara hiyo inahudumia usafiri wa mizigo na abiria kutoka karibu mikoa yote ya Tanzania pamoja na mataifa jirani zaidi ya nane, hivyo kuwa kiungo muhimu cha biashara na uchumi wa kikanda.

Dkt.Temba amesisitiza kuwa,uboreshaji wa barabara hiyo utasaidia kupunguza ajali, kuongeza ufanisi wa usafiri na kuimarisha maendeleo ya kiuchumi kwa wananchi na taifa kwa ujumla.

Amesema kuwa, licha ya uwepo wa reli ya kisasa ya mwendo kasi, barabara bado inaendelea kuwa mhimili mkuu wa usafiri na usafirishaji nchini. 

Inakadiriwa kuwa, zaidi ya asilimia 70 ya huduma za kijamii na kiuchumi hutegemea usafiri wa barabara, ikilinganishwa na huduma za reli ambazo kwa sasa zinahudumia maeneo machache katika kanda maalumu.

Barabara ya Morogoro, ambayo ni mojawapo ya barabara kuu inayounganisha mikoa na nchi jirani, imeelezwa kuwa na umuhimu mkubwa katika uchumi wa taifa kutokana na mchango wake katika usafirishaji wa watu na mizigo.

Kutokana na umuhimu huo, Dkt.Temba amependekeza kuimarishwa kwa mifumo ya usalama barabarani, ikiwemo uwekaji wa uzio maalumu katika maeneo hatarishi ya barabara kuu. 

Hatua kama hizo, amesema tayari zimetekelezwa katika baadhi ya nchi za Kusini mwa Afrika kama Zimbabwe, Botswana, Namibia na Afrika Kusini, ambapo barabara kuu zimewekewa uzio kwa lengo la kuimarisha usalama wa watumiaji wa barabara na kulinda miundombinu hiyo muhimu.

Pia, amesema Tanzania inaweza kujifunza kutoka mifano hiyo ili kuimarisha zaidi usalama wa miundombinu ya usafiri, sambamba na maendeleo yanayoendelea katika sekta ya reli ya mwendo kasi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here