ZANZIBAR-Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Alhaj Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amejumuika na viongozi mbalimbali wa Serikali, wanafamilia pamoja na wananchi katika mazishi ya Ndugu Hamza Khamis Hamza, aliyefariki jana.
Marehemu Hamza Khamis Hamza (75) amefariki jana alipokuwa akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Mkoa ya Lumumba, Mkoa wa Mjini Magharibi.
Maziko hayo yamefanyika leo Machi 13,2026 katika eneo la Mlandege. Marehemu ni baba mzazi wa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Mheshimiwa Khamis Hamza Khamis Chillo.
Mapema, Rais Dkt. Mwinyi alijumuika na waumini wa dini ya Kiislamu katika ibada ya Sala ya Ijumaa pamoja na Sala ya Jeneza iliyosaliwa katika Msikiti wa Salaam uliopo Mlandege, Mkoa wa Mjini Magharibi.
Marehemu amezikwa kijijini kwao Kidimni, Wilaya ya Kati, Mkoa wa Kusini Unguja. Mwenyezi Mungu amlaze mahala pema Peponi, Ameen.




