Rais Dkt.Samia afungua milango,Italia yaleta Kiwanda cha Chuma cha trilioni 4.2 Mtwara

DAR-Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan leo Machi 29,2026 Ikulu jijini Dar es Salaam amekutana na Balozi wa Italia nchini Tanzania, Mheshimiwa Giuseppe Sean Coppola.
Kwa pamoja viongozi hao wamejadili mradi wa ujenzi wa kiwanda kikubwa na cha kisasa cha chuma Mtwara, kwa kushirikiana na mwekezaji mzawa.

Mradi huo, wenye thamani ya takribani Euro bilioni 1.5 (sawa na takribani Shilingi trilioni 4.2 za Kitanzania), unatarajiwa kuanza kutekelezwa hivi karibuni.

Rais Dkt. Samia amesema,Tanzania inaendelea kujijenga kama kituo shindani na cha kuaminika kwa uwekezaji, ikitegemea rasilimali zake asilia, nafasi yake ya kimkakati, pamoja na mageuzi yanayoendelea kuboresha mazingira ya biashara.

Ameeleza kuwa,mradi huu ni matokeo ya ziara yake nchini Italia, ambapo alishiriki katika maonesho ya kimataifa ya nishati, maji na ujenzi (Ecomondo) na kukutana na wawekezaji kutoka Italia.
Rais Dkt.Samia amewahakisha wawekezaji wa Italia kuwa,Serikali ya Tanzania ipo tayari kuwaunga mkono katika shughuli zao na kuwezesha utekelezaji wa miradi yao kwa ufanisi.

Nchi ya Italia ni mshirika muhimu wa Tanzania katika maendeleo, hasa katika sekta ya viwanda, nishati na miundombinu.

"Tunakaribisha ushirikiano unaoongeza thamani ya rasilimali zetu, unaozalisha ajira kwa wananchi wetu, na kuchangia dira yetu ya muda mrefu ya kujenga uchumi wa viwanda.”

Kwa upande wake, Balozi wa Italia ameeleza kuwa, ushirikiano huo unaakisi kuimarika kwa mahusiano ya kiuchumi kati ya Tanzania na Italia chini ya mifumo mipana ya ushirikiano wa maendeleo.

“Nia iliyooneshwa na Danieli Group ni sehemu ya juhudi pana za kuimarisha ushirikiano kati ya nchi zetu mbili, ikiwemo kupitia Mpango wa Mattei kwa Afrika.
"Mpango huu unalenga kukuza uwekezaji endelevu wa wenye manufaa kwa pande zote, na Tanzania inaonekana kuwa mshirika muhimu katika muktandha huu. Kwa sasa, tupo katika hatua ya kuangalia uwezekano na kutarajia kuendelea kushirikiana kwa karibu na Serikali ya Tanzania kadri majadiliano yatakavyoendelea,”amesisitiza Balozi huyo.

Naye Mtendaji Mkuu wa Danieli Group, Bw. Giacomo Mareschi Danieli ameeleleza sababu za kimkakati zilizofanya kampuni hiyo kuvutiwa na Tanzania.

“Tunaona fursa kubwa nchini Tanzania, si tu kutokana na uwepo wa rasilimali kama gesi na madini ya chuma, bali pia kutokana na ukuaji wa soko na nafasi yake ya kimkakati katika ukanda huu.

“Mtazamo wetu unalenga ushirikiano wa muda mrefu,kuleta teknolojia ya kisasa inayozingatia mazingira, huku tukishirikiana na wadau wa ndani kukuza ujuzi na kujenga uwezo endelevu wa viwanda. Hii ni hatua ya awali, na tumejiunga kuendelea na majadiliano ya kitaalumu ili kutathmini uwezekano wa mradi huu,” ameongeza.
Iwapo utatekelezwa, uwekezaji huu unatarajiwa kuchangia kwa kiasi kikubwa katika ajenda ya Tanzania ya kujenga uchumi wa viwanda chini ya Dira ya Taifa ya 2050, kwa kuimarisha uzalishaji wa ndani wa chuma, kupunguza uagizaji kutoka nje, kuongeza thamani ya rasilimali za ndani, na kutengeneza ajira kwa vijana.

Aidha, unaweza kuimarisha nafasi ya Tanzania kama kitovu cha uzalishaji wa chuma katika ukanda huu, hususan kwa nchi jirani zisizo na bandari, pamoja na kusaidia maendeleo ya miundombinu na usafirishaji katika ukanda wa Mtwara.

Mheshimiwa Rais Samia amemhakikishia Mheshimiwa Balozi na ujumbe wake kuwa, Serikali itaendelea kuwa wazi kwa wawekezaji wenye sifa, na si wanaoleta mtaji pekee bali pia teknolojia, ujuzi na dhamira ya muda mrefu katika maendeleo ya Tanzania.
Kikao hicho kimeonesha kuendelea kuimarika kwa mvuto wa Tanzania kama kitovu cha uwekezaji, pamoja na dhamira ya pamoja ya pande zote mbili kuendelea kuchangia fursa zitakazozalisha thamani endelevu ya kiuchumi na ukuaji shirikishi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here