Sera imara za kiuchumi zachochea ukuaji wa uchumi Tanzania, Gavana Tutuba awapongeza viongozi wakuu

NA GODFREY NNKO

GAVANA wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT),Bw. Emmanuel Tutuba amemshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuendelea kuwaongoza katika utekelezaji wa majukumu yao ya kusimamia uchumi wa nchi na sekta ya fedha, akisisitiza kuwa mafanikio yaliyopatikana yametokana na uongozi thabiti wa viongozi wakuu wa nchi.
Ameyasema hayo Machi 6,2026 katika hafla ya Futari iliyoandaliwa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) katika makao makuu ndogo jijini Dar es Salaam ambayo iliwakutanisha wadau,viongozi na wananchi mbalimbali mkoani Dar es Salaam.

Akizungumza kuhusu hali ya uchumi, Gavana Tutuba ameeleza kuwa, chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt.Samia Suluhu Hassan, pamoja na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt.Hussein Ali Mwinyi, nchi imeendelea kusimamia vyema uchumi wake na kuhakikisha sekta ya fedha inaendelea kuwa imara.
Amesema,sekta ya fedha nchini imeendelea kuwa na mtaji na ukwasi wa kutosha, hali inayoiwezesha kujiendesha kwa ufanisi na faida huku ikiendelea kukua kwa kasi ya kuridhisha.

“Tunaendelea kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuwa, kwa kuzingatia vigezo vya kitaifa na kimataifa,Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazofanya vizuri kiuchumi duniani. Kwa mujibu wa takwimu za mwaka 2025, uchumi wa Tanzania uliendelea kukua kwa wastani wa asilimia 6, huku Zanzibar ikifikia ukuaji wa asilimia 6.8,” amesema Gavana Tutuba.

Ameongeza kuwa, matarajio ya mwaka 2026 yanaonesha kuwa, uchumi wa Tanzania Bara utakua kwa asilimia 6.3, wakati uchumi wa Zanzibar unatarajiwa kukua kwa asilimia 7.2.
Kwa mujibu wa Gavana huyo, mwenendo huo chanya wa ukuaji wa uchumi unachochewa na utekelezaji mzuri wa sera madhubuti za kiuchumi, zikiwemo sera za fedha, sera za kodi pamoja na sera za matumizi ya umma.

Aidha, amebainisha kuwa, kuboreshwa kwa mazingira ya biashara nchini kumechangia pia ukuaji wa uchumi, sambamba na kuongezeka kwa mauzo ya bidhaa nje ya nchi.

Miongoni mwa bidhaa hizo ni madini ya dhahabu pamoja na mazao ya biashara kama korosho na kahawa, huku sekta ya utalii ikiendelea kukua kutokana na ongezeko la idadi ya watalii.

Katika eneo la mfumuko wa bei, Gavana Tutuba amesema mamlaka zimefanikiwa kuudhibiti ndani ya kiwango kilichowekwa.

“Katika eneo hili tumefanikiwa kulisimamia vizuri na kuhakikisha kunakuwepo na utulivu wa bei. Kwa sasa mfumuko wa bei unaendelea kuwa ndani ya lengo tulilojiwekea la kati ya asilimia 3 hadi 5,”ameeleza Gavana Tutuba.

Amefafanua kuwa, kwa mwaka 2025, kiwango cha wastani cha mfumuko wa bei kilikuwa asilimia 3.3 kwa Tanzania Bara na asilimia 3.7 kwa upande wa Zanzibar.
Kwa mujibu wa Gavana huyo, mafanikio hayo yametokana na utekelezaji thabiti wa sera ya fedha, utulivu wa bei za vyakula, uthabiti wa viwango vya ubadilishaji wa fedha pamoja na kushuka kwa bei za mafuta katika soko la dunia na kupungua kwa bei za vyakula katika baadhi ya nchi jirani.

Pia, amesisitiza kuwa, BoT itaendelea kusimamia kwa karibu sera za fedha ili kuhakikisha uchumi wa nchi unaendelea kukua kwa kasi endelevu na kuimarisha ustawi wa sekta ya fedha nchini.

Awali, kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mheshimiwa Albert Chalamila, Mstahiki Meya wa Manispaa ya Temeke, Mheshimiwa Uzairu Abdul Athumani amesema kuwa, Ramadhani ni mwezi wa toba na kujitafakari huku akisisitiza kuwa, kuyatenda hayo kunarejesha uadilifu na uwajibikaji kwa kila mmoja kwa manufaa ya jamii na Taifa kwa ujumla.
Pia, amesisitiza kuwa, mafunzo na tafakari ambazo kila mmoja anapata katika mfungo huu yasiishie katika mwezi huu bali yaende katika miezi inayokuja ili yawe mbegu bora kwa Taifa.

"Ni matumaini ya Serikali kuwa, mambo haya mazuri tunayoyasoma katika mwezi huu yataisaidia jamii ya Watanzania, Waislamu na wasiokuwa Waislamu ili kuongeza ustaarabu, nidhamu na uadilifu kwenye kila njanja ya maisha yetu."

Amesisitiza kuwa, kukosekana kwa uadilifu kumekuwa ni changamoto kubwa kwa Taifa, hivyo baada ya mfungo kila mmoja akayaishi mafunzo aliyoyapata ambayo yamejikita katika kuimarisha uadilifu kwa kila mmoja.

Kwa niaba ya Mufti wa Tanzania na Sheikh Mkuu, Dkt.Abubakari Zuberi, Mkurugenzi wa Mambo ya Nje wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) makao makuu, Twahir Al-musawaa ameipongeza BoT kwa kuandaa hafla hiyo ambayo inaonesha mshikamano, upendo na huruma kati ya Watanzania.
"Lakini,ninapenda pia kupongeza Benki Kuu ya Tanzania kwa kuandaa Futari hii,kitendo hiki kinaonesha wazi moyo wa ushirikiano na heshima kwa waumini wa dini ya Kiislamu katika Mwezi huu Mtukufu wa Ramadhani, ni ishara kwamba taasisi zetu za Kitaifa zinathamini umoja na zinaamini katika kuleta umoja na mshikamano kwa Watanzania bila kujali tofauti zetu,za kidini au za kijamii.

"Hatua hii ya Benki Kuu ya Tanzania inaonesha kuwa, katika Taifa letu hakuna ubaguzi, sisi sote ni Watanzania, tunashirikiana na kujenga nchi yetu kwa manufaa ya Taifa letu."
Pia, amesema Mwezi Mtukufu unafundisha maadili mema huku ukikumbusha kila mmoja umuhimu wa uadilifu, uwajibikaji, huruma, kusaidiana na kujenga mahusiano mema kati yetu, mambo ambayo amesisitiza ni muhimu kwa ustawi wa jamii na Taifa kwa ujumla.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here