Serikali kuimarisha miundombinu kuzunguka uwanja wa AFCON Arusha

ARUSHA-Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Paul Christian Makonda (Mb) amesema Serikali imetoa maelekezo maalum ya kuharakisha ujenzi wa miundombinu ya barabara itakayorahisisha upatikanaji wa Uwanja wa Mpira wa Miguu wa AFCON Arusha.
Akizungumza mbele ya Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo wakati wa ukaguzi wa mradi huo, Mhe. Makonda amesema barabara zilizo chini ya usimamizi wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) zitakuwa sehemu muhimu ya kuunganisha wananchi na uwanja huo.

Ameeleza kuwa tarehe 18 ya mwezi huu Serikali itasaini mkataba wa ujenzi wa kilometa 13 za barabara zitakazounganisha maeneo mbalimbali na kuwaleta wananchi moja kwa moja katika uwanja huo, ambapo mkandarasi anatarajiwa kuanza kazi mara moja baada ya kusainiwa kwa mkataba.

Kwa mujibu wa Waziri Makonda, uwanja huo utakuwa na barabara nne za kuingia na kutoka, hatua itakayosaidia kupunguza msongamano wa magari wakati wa matukio makubwa ya michezo. Aidha, kutajengwa roundabout na barabara za mzunguko zitakazorahisisha mtiririko wa magari kuingia na kutoka katika eneo la uwanja.

Katika hatua nyingine, Mhe. Makonda amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, pia ameagiza Wizara ya Ujenzi kujenga barabara nyingine zitakazosaidia kupunguza msongamano wa magari katikati ya Jiji la Arusha.

Ameongeza kuwa tayari mkataba wa kwanza wa ujenzi wa barabara nyingine za kilometa 12 umesainiwa, na mkandarasi ameanza maandalizi ya awali ya ujenzi ikiwemo kuweka kambi ya kazi, barabara ambazo zitaunganishwa na zile za TARURA ili kurahisisha zaidi upatikanaji wa uwanja.

Mhe. Makonda amesisitiza kuwa uwekezaji huo unaonesha dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kuhakikisha si tu uwanja wa kisasa unajengwa, bali pia miundombinu inayouzunguka inaboreshwa ili mashabiki na wadau wa michezo waweze kufika kwa urahisi.

Aidha, amesema katika hatua zinazofuata baada ya kukamilika kwa uwanja huo, Serikali inapanga kuendeleza eneo hilo kuwa Sport Park, kwa kujenga miundombinu ya michezo mingine ili kuwezesha michezo mbalimbali kufanyika katika eneo moja.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here