ARUSHA-Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Paul Christian Makonda (Mb) amesema Serikali inalenga kufanya mpira wa miguu kuwa sehemu ya kukuza utalii nchini, huku Mkoa wa Arusha ukitajwa kuwa moja ya maeneo muhimu yatakayonufaika na mkakati huo.
Akizungumza mbele ya Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo wakati wa ukaguzi wa mradi wa ujenzi wa Uwanja wa Mpira wa Miguu wa Kimataifa wa Arusha, Mhe. Makonda amesema maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ni kuhakikisha michezo inatumika kama kichocheo cha utalii na ukuaji wa uchumi wa maeneo mbalimbali nchini.
Ameeleza kuwa pamoja na ujenzi wa uwanja wa kisasa unaokadiriwa kugharimu karibu Shilingi Bilioni 300, Serikali pia inapanga kuimarisha miundombinu ya mikutano kwa kujenga kituo kikubwa cha mikutano (Conference Centre) chenye thamani ya takribani Shilingi Bilioni 400, ili kuwezesha Arusha kuwa kitovu cha mikutano mikubwa ya kimataifa na kikanda katika ukanda wa Afrika Mashariki.
Aidha, mpango huo pia unajumuisha ujenzi wa hospitali maalum kwa ajili ya utalii wa matibabu, hatua inayolenga kuongeza huduma bora kwa wageni na washiriki wa matukio makubwa ya kimataifa watakaotembelea eneo hilo.
Kwa mujibu wa Waziri Makonda, uwekezaji huo wa miundombinu ya michezo, mikutano na huduma za afya unatarajiwa kusaidia kuongeza mafanikio ya Uwanja wa Mpira wa Miguu wa Kimataifa wa Arusha na kuifanya Arusha kuwa kitovu muhimu cha michezo, utalii na mikutano katika kanda.
