NA GODFREY NNKO
SERIKALI imeeleza mafanikio makubwa yaliyopatikana katika sekta za uchukuzi, reli, bandari, usafiri wa majini na utalii katika kipindi cha siku 100 za uongozi wa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan, ikisisitiza kuwa uwekezaji mkubwa wa miundombinu umeanza kuzaa matunda kiuchumi.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali,Bw. Gerson Msigwa akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) kuhusu utendaji wa serikali katika siku 100 za uongozi wa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan. Ni Februari 26, 2026 katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.
Hayo yamesemwa Februari 26,2026 na Msemaji Mkuu wa Serikali, Bw. Gerson Msigwa wakati akizungumza na waandishi wa habari wa vyombo vya habari mbalimbali nchini katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.
Msigwa ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo alikuwa akizungumzia kuhusu utendaji wa Serikali katika siku 100 za uongozi wa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan.
Amesema,mchango wa sekta ya uchukuzi katika Pato la Taifa umeongezeka kutoka asilimia 7.1 mwaka 2021 hadi asilimia 7.5 mwaka 2024, ikiwa ni matokeo ya utekelezaji wa miradi ya kimkakati kote nchini.
MIRADI YA KIMKAKATI INAYOENDELEA KUTEKELEZWA
Katika kipindi cha kuanzia mwaka 2022/23 hadi 2024/25, Msigwa amesema,Serikali imeendelea kutekeleza miradi mbalimbali katika viwanja vya ndege yenye thamani ya shilingi trilioni 1.154 inayolenga kuongeza uwezo wa viwanja hivyo kuhudumia ndege, abiria na mizigo na kuboresha usalama, ulinzi na uwezeshaji katika Viwanja hivyo.
Baadhi ya miradi iliyotekelezwa katika kipindi hicho imekamilika kwa asilimia 100 na mingine ipo hatua za mwisho za ukamilishwaji.
Kuhusu kiwanja cha ndege cha Arusha, Msigwa amesema, Serikali kupitia Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) inaendelea kutekeleza mradi wa uwekaji taa za kuongozea ndege (AGL), unaogharamiwa na Serikali pamoja na ujenzi wa kituo cha umeme kwa gharama ya Shilingi bilioni 10.472.
Mradi huu kwa sasa umefikia asilimia 25 ya utekelezaji. Aidha, ujenzi wa jengo la abiria katika uwanja huu ulikwishakamilika na jengo hilo linatumika.
Kiwanja cha ndege cha Moshi, amesema Serikali kupitia TAA inatekeleza mradi wa ukarabati na upanuzi wa kiwanja cha ndege cha Moshi ambao kwa sasa unaendelea kwa gharama ya shilingi bilioni 14.14.
Mradi huu unahusisha ukarabati wa barabara ya kuruka na kutua ndege kwa kiwango cha lami yenye urefu wa mita 1,240, ujenzi wa barabara za kuingia kiwanjani zenye urefu wa mita 455.3, ujenzi wa maegesho ya ndege na njia za kiunganishi kwa kiwango cha lami, pamoja na ujenzi wa barabara za mzunguko na uzio wa usalama wenye urefu wa kilometa 8. Mradi huu umefikia asilimia 69 ya utekelezaji.
Aidha,Kiwanja cha ndege cha Mwanza, amesema, kazi ya upembuzi yakinifu na Usanifu wa Kina wa Ujenzi wa Jengo Jipya la Abiria na miundombinu yake unaendelea na taarifa ya awali imekwishakamilika na sasa ipo katika hatua ya maboresho ili utekelezaji wake uanze.
Kiwanja kipya cha ndege cha Serengeti, amesema kuwa,Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) inafanya Upembuzi yakinifu na Usanifu wa Kina wa Kiwanja Kipya cha Kimataifa cha Ndege Serengeti.
Kazi hiyo inahusisha usanifu wa miundombinu ya kiwanja cha ndege, usanifu wa jengo la abiria, jengo la mizigo na mfumo wa taa za kuongozea ndege.
"Jambo muhimu kwenye utekelezaji wa mradi huu ni kwamba umezingatia kwa kina utunzaji wa ikolojia ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, kuhakikisha maendeleo ya miundombinu ya anga hayaathiri mazingira na urithi wa asili wenye hadhi ya kimataifa."
Kiwanja kipya cha ndege cha Kyabajwa (Kagera), Msigwa amesema upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa Kiwanja Kipya cha Ndege cha Kyabajwa Kagera unaendelea unahusisha usanifu wa miundombinu ya kiwanja, jengo la abiria, jengo la mizigo, taa za kuongozea ndege, pamoja na usanifu wa uzio wa usalama, kituo cha umeme na kituo cha zimamoto na uokoaji.
Kiwanja cha ndege cha Kimataifa cha Msalato,amesema mradi huu unajengwa kwa ufadhili wa Benki ya Maendeleo Afrika (AfDB) na umegawanyika katika sehemu mbili ambapo sehemu ya kwanza inahusisha ujenzi wa barabara ya kuruka na kutua ndege, maegesho ya ndege, barabara za kuingia na kutoka kiwanjani, barabara za viungio, usimikaji wa taa za kuongozea ndege na ujenzi wa uzio wa usalama kwa gharama ya shilingi bilioni 165.627, ukitekelezwa na Sinohydro na umefikia asilimia zaidi ya 90.
Sehemu ya pili inahusisha ujenzi wa jengo la abiria, maegesho ya magari, kituo cha umeme na miundombinu saidizi kwa gharama ya shilingi bilioni 194.403, ukitekelezwa na Beijing Engineering na umefikia asilimia 68.
Kiwanja cha ndege cha Shinyanga, amesema kuwa, Mradi wa Ukarabati na Upanuzi wa Kiwanja cha Ndege cha Shinyanga unaendelea kwa ufadhili wa Benki ya Uwekezaji ya Ulaya (EIB) ukihusisha ujenzi wa barabara ya kuruka na kutua ndege yenye uwezo wa kupokea ndege aina ya Bombardier Q400, ujenzi wa jengo la abiria lenye uwezo wa kuhudumia abiria 250,000 kwa mwaka, ujenzi wa maegesho ya ndege, njia unganishi, maegesho ya magari, mifereji ya maji ya mvua, kituo cha umeme na uzio wa usalama.
Kiwanja cha ndege cha Tabora, mradi wa ukarabati na upanuzi wa Kiwanja cha Ndege cha Tabora kwa sasa umefikia asilimia 98. Mradi huu umekamilisha jengo la abiria ambalo limeanza kutumika kwa ufadhili wa Benki ya Uwekezaji ya Ulaya (EIB) kwa gharama ya shilingi bilioni 26.1.
Mradi huu unahusisha ujenzi wa jengo la abiria lenye uwezo wa kuhudumia abiria 500,000 kwa mwaka lililounganishwa na mnara wa kuongozea ndege, maegesho ya magari, barabara za kuingia kiwanjani, kituo cha hali ya hewa na uzio wa usalama wenye urefu wa mita 8,250.
Kiwanja cha ndege cha Kigoma; Mradi huu kwa sasa umefikia asilimia 42 ukijengwa kwa ufadhili wa Benki ya Uwekezaji ya Ulaya, European Investment Bank (EIB) kwa gharama ya shilingi bilioni 46.68 Mradi wa Ujenzi wa Jengo la Abiria katika Kiwanja cha Ndege cha Kigoma unaendelea ukihusisha ujenzi wa jengo la abiria lenye uwezo wa kuhudumia abiria 400 kwa wakati mmoja, upanuzi wa maegesho ya ndege, ujenzi wa mnara wa kuongozea ndege, kituo cha umeme, maegesho ya magari, barabara za kuingia kiwanjani na uzio wa usalama pamoja na mfumo wa taa za kuongozea ndege.
Kiwanja cha ndege cha Sumbawanga, Mradi huu upo katika hatua za mwishoni ukihusisha ukarabati na Upanuzi wa Kiwanja cha Ndege cha Sumbawanga ukitekelezwa kwa wa ufadhili wa Benki ya Uwekezaji ya Ulaya (EIB) kwa gharama ya shilingi bilioni 60.101, ukitekelezwa na Beijing Construction Engineering Group.
Mradi unahusisha ujenzi wa jengo la abiria lililounganishwa na mnara wa kuongozea ndege, ujenzi wa barabara ya kuruka na kutua ndege daraja pamoja na mfumo wa taa za kuongozea ndege kwa huduma za saa 24, maegesho ya magari, kituo cha hali ya hewa na uzio wa usalama.
Aidha, Serikali imekamilisha jengo la Viongozi Mashuhuri katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, hatua itakayoongeza hadhi ya nchi kidiplomasia.
MAZINGIRA SALAMA YA UWEKEZAJI KWA MASHIRIKA YA NDEGE
Msigwa amesema, Serikali imeendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji katika sekta ya anga kwa kuimarisha miundombinu ya viwanja vya ndege ili kukidhi viwango vya kimataifa pia kukuza utalii na biashara kwa kuimarisha usalama na utulivu.
Katika eneo hili, amesema Wizara ya Uchukuzi kupitia Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Nchini (TAA) imefanikiwa kuvutia mashirika mapya saba (7) ya ndege ya kimataifa kuanzisha safari nchini.
Mashirika hayo ni Airlink, Zambia Airways, Saudia,Air France,Skyward Express,South African Airways na Xerin Air.
Hatua hii imeongeza ushindani wa kibiashara, kurahisisha safari za kimataifa na kuchochea ukuaji wa utalii na biashara.
Aidha, kutokana na maboresho ya miundombinu na mifumo ya usalama, Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro vimetambuliwa kimataifa kwa tuzo za ubora na usalama, jambo linaloimarisha hadhi ya Tanzania katika sekta ya anga.
TAKWIMU ZA SAFARI ZA NDEGE, ABIRIA NA MIZIGO
Msemaji Mkuu wa Serikali amesema kuwa, Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) imeendelea kukusanya na kuchambua takwimu rasmi za uendeshaji wa viwanja vya ndege 61 inavyovisimamia.
Takwimu hizi zinahusu idadi ya safari za ndege, abiria na tani za mizigo, na hutumika kama kiashiria muhimu cha kupima uimara wa sekta ya usafiri wa anga pamoja na kusaidia maamuzi ya uwekezaji, ukarabati, upanuzi na uboreshaji wa viwanja vya ndege.
Ulinganisho wa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na 2023/2024
1. Safari za Ndege
2023/2024: Safari 148,897
2024/2025: Safari 149,835
Ongezeko: Asilimia 0.6
2. Idadi ya Abiria
2023/2024: Abiria milioni 5.15
2024/2025: Abiria milioni 5.25
Ongezeko: Asilimia 2.0
3. Tani za Mizigo
2023/2024: Tani 34,620
2024/2025: Tani 37,683
Ongezeko: Asilimia 8.8
Takwimu zinaonesha kuwa, licha ya ongezeko dogo la safari za ndege, kumekuwa na ukuaji mkubwa zaidi katika idadi ya abiria na hasa mizigo, jambo linaloashiria kuimarika kwa shughuli za kiuchumi na biashara zinazotegemea usafiri wa anga.
Mwenendo wa Julai Disemba 2025 ikilinganishwa na Julai Disemba 2024
Katika kipindi cha nusu mwaka (JulaiDisemba 2025), sekta imeendelea kuimarika kama ifuatavyo:
Safari za Ndege
JulaiDisemba 2024: 83,647
JulaiDisemba 2025: 91,760
Ongezeko: Asilimia 10
Abiria
JulaiDisemba 2024: 2,819,912
JulaiDisemba 2025: 3,071,081
Ongezeko: Asilimia 9
Hali hii inaonesha mwelekeo chanya wa ukuaji unaoendelea, unaochochewa na kuimarika kwa shughuli za usafiri wa ndani na kimataifa, pamoja na kuongezeka kwa mahitaji ya huduma za usafiri wa anga.
"Kwa ujumla, takwimu hizi zinaonesha kuimarika kwa sekta ya usafiri wa anga nchini na kutoa msingi mzuri wa mipango ya maendeleo ya baadaye ya viwanja vya ndege."
TAKWIMU MUHIMU ZA UTENDAJI
Msigwa anasema, uwekezaji huu wa Serikali umeiwezesha ATCL kuongeza uwezo wa utoaji huduma na kuchangia ongezeko la abiria kutoka 822,232 waliosafirishwa mwaka 2021/22 hadi kufikia abiria 1,178,025 mwaka 2024/25.
Aidha, katika kipindi cha nusu mwaka pekee (JulaiDesemba 2025), ATCL ilisafirisha abiria 709,432.
Usafirishaji wa mizigo umeongezeka kutoka tani 2,567 mwaka 2021/22 hadi tani 6,919 mwaka 2024/25.
Ongezeko hili limechangiwa na Serikali kununua ndege ya mizigo na kuwezesha upanuzi wa safari za kimataifa na kikanda, hatua iliyorahisisha usafirishaji wa mazao ya kilimo, mifugo, mbogamboga na matunda kwenda masoko ya nje.
Pia, amesema, mchango wa ATCL katika uchumi wa Taifa umeongezeka. ATCL imekusanya Dola za Marekani milioni 157.69 katika kipindi cha mwaka 2024/25 sawa na ongezeko la asilimia 87.88 ikilinganishwa na mwaka uliotangulia.
Aidha, katika mwaka 2024/25 ATCL imefanikiwa kuchangia Shilingi bilioni 52.35 kama kodi, ada na tozo mbalimbali za kisheria.
Kampuni pia imepanga kuanzisha safari za Seychelles, Muscat na Jeddah kabla ya Juni 2026, hatua itakayofungua fursa zaidi za biashara kimataifa.
ATCL imeongeza ajira kwa Watanzania, kutoka 826 Juni, 2024 hadi watumishi 1,031 mwezi Disemba, 2025. Pia, watumishi 356 wameendelezwa kwa kupatiwa mafunzo maalum ili kuongeza ujuzi na tija katika kada za urubani, uhandisi wa ndege, na masuala muhimu ya usafiri wa anga.
UJENZI NA UENDESHAJI WA RELI YA KATI (SGR)
Serikali kupitia Shirika la Reli Tanzania (TRC) imeendelea na ujenzi wa Reli ya Kisasa (Standard Gauge Railway SGR) kwa awamu ya kwanza kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza yenye jumla ya kilomita 1,219 za njia kuu na kilomita 377 za njia za kupishania.
Awamu hii imegawanyika katika vipande vitano ambavyo ni Dar es Salaam Morogoro (Km 300),Morogoro Makutupora (Km 422),
Makutupora Tabora (Km 368),Tabora Isaka (Km 165) na Isaka Mwanza (Km 341).
Utekelezaji wa kipande cha Dar es Salaam hadi Dodoma umekamilika na huduma zinaendelea kutolewa, huku kipande cha kuingia bandarini kikiwa kimefikia asilimia 99.93.
Aidha, ujenzi wa awamu ya pili unaendelea katika vipande vya Tabora Kigoma (Km 506) na Uvinza Musongati (Km 300).
Hadi kufikia Desemba 2025, Msigwa amesema kuwa, utandazaji wa reli ya SGR umefikia kilomita 747, sawa na asilimia 61 ya lengo la kilomita 1,219 ifikapo mwaka 2025/26.
Utandazaji wa reli ni hatua ya mwisho baada ya kazi za ujenzi wa tuta, ufyatuaji wa mataruma, ujenzi wa madaraja na miundombinu mingine.
HALI YA UTEKELEZAJI WA VIPANDE VYA SGR:
Dar es Salaam Morogoro (Km 300): 99.93%
Morogoro Makutupora (Km 422): 98.60%
Makutupora Tabora (Km 368): 14.54%
Tabora Isaka (Km 165): 8.95%
Mwanza Isaka (Km 341): 67.85%
Tabora Kigoma (Km 506): 9.06%
MAFANIKIO YA UENDESHAJI WA SGR
Amesema, huduma za treni ya SGR kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma zimepunguza muda wa safari kutoka saa 1012 kwa mabasi hadi saa 34 kwa treni.
Tangu kuanza kwa huduma hadi Desemba 2025 amesema,abiria 4,665,004 wamesafirishwa huku tani 52,305 za mizigo zikisafirishwa na
Watanzania 207,468 wamepata ajira.
Kati ya ajira hizo, Msigwa amesema kuwa,1,304 wameajiriwa katika vituo vya SGR, 55,284 ajira za moja kwa moja na 150,880 ajira zisizo za moja kwa moja.
Huduma ya SGR imeongeza tija katika uchumi, biashara na utalii, hususan kwa wasafiri wanaoelekea maeneo ya hifadhi kama Mikumi, Ruaha na Udzungwa.
Katika mwaka 2024/25 na nusu ya 2025/26, Wizara ya Uchukuzi imekamilisha Upembuzi Yakinifu wa reli za mijini katika Jiji la Dar es Salaam na Dodoma, hatua iliyopelekea kupatikana kwa fedha za msaada kwa ajili ya usanifu wa kina.
Kuanzia Desemba 2025, TRC imeanza kujiendesha bila ruzuku ya mishahara ya takribani shilingi bilioni 13 kwa mwaka iliyokuwa ikitolewa kwa takribani miaka 13.
Aidha, TRC imeanzisha kampuni tanzu ya Tanzania Railway Limited inayomilikiwa kwa asilimia 100 na TRC kwa lengo la kuongeza ufanisi wa kibiashara na mapato.
UKARABATI WA RELI YA MGR
Msigwa amesema, Serikali imeendelea kuboresha reli ya zamani (MGR) kwa kuondoa reli za ratili 45 na kuweka ratili 80.
Pia, kuongeza uwezo wa madaraja kutoka ekseli 13.5 hadi 18.5 na kusaini mkataba wa ukarabati wa kipande cha Tabora Kigoma (Km 411).
UNUNUZI WA MABEHEWA, VICHWA NA VITENDEA KAZI
Hadi Juni 2026, TRC inakusudia kuwa na jumla ya vitendea kazi 59 (vichwa vya treni na mabehewa).
Msigwa amesema, hatua zilizochukuliwa ni pamoja na:
(i) Kwa Reli ya MGR:
Ununuzi wa mabehewa 100 ya mizigo
Ununuzi wa vichwa 8 vya treni (2 vimewasili na vipo majaribioni)
Uundwaji wa vichwa 6 katika karakana ya Pugu (kukamilika Machi 2026)
(ii) Kwa Reli ya SGR:
Vichwa 17 vya umeme
Seti 10 za treni za umeme
Mabehewa 89 ya abiria
Mitambo ya matengenezo 24
Mabehewa 1,430 ya mizigo (264 yamewasili hadi Desemba 2025).
(iii) Ukarabati wa Vitendea Kazi:
Vichwa 9 vya treni vimekarabatiwa
Mabehewa 37 ya abiria
Mabehewa 368 ya mizigo
RELI YA TAZARA
Serikali kupitia Wizara ya Uchukuzi imepiga hatua kubwa katika kufufua TanzaniaZambia Railway Authority.
Mkataba wa ufufuaji na uboreshaji mkubwa wa reli ya TAZARA ulisainiwa tarehe 29 Septemba 2025 kati ya Serikali za Tanzania na Zambia kwa kushirikiana na Kampuni ya CCECC ya China.
Uzinduzi wa mradi ulifanyika tarehe 20 Novemba 2025 nchini Zambia, na utekelezaji rasmi unatarajiwa kuanza Juni 2026.
Amesema, mradi huu unatarajiwa kuongeza ufanisi wa Bandari ya Dar es Salaam na
kuimarisha biashara kati ya Tanzania na nchi za SADC ikiwemo kufungua fursa za ajira na ukuaji wa uchumi katika mikoa inayopitiwa na reli
"Kwa ujumla, mafanikio haya katika sekta ya reli ni hatua ya kihistoria chini ya uongozi wa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, yakionesha dhamira ya Serikali ya kuimarisha miundombinu ya usafiri kwa maendeleo ya taifa."
UENDELEZAJI WA BANDARI NA USAFIRI WA MAJINI
Katika kipindi cha mwaka 2024/25 na nusu ya mwaka 2025/26, Serikali imeendelea kufanya uwekezaji mkubwa katika sekta ya bandari na usafiri majini kama mhimili muhimu wa biashara ya ndani, kikanda na kimataifa.
UPANUZI WA BANDARI YA DAR ES SALAAM
Msigwa amesema, wizara imekamilisha taratibu za kuanza upanuzi mkubwa wa Bandari ya Dar es Salaam unaojumuisha ujenzi wa magati 10 mapya, ujenzi wa matenki 15 ya kupokelea mafuta yenye ujazo wa mita za ujazo 378,000.
Ujenzi wa magati mawili ya awali yenye urefu wa mita 500 unatarajiwa kuanza Juni, 2026, huku ujenzi wa matenki ukiendelea vizuri.
Amesema,maboresho haya yataongeza uwezo wa bandari kuhudumia hadi tani milioni 50 kwa mwaka kutoka wastani wa tani milioni 32 za sasa.
UJENZI WA BANDARI YA BAGAMOYO
Serikali imeanza maandalizi ya ujenzi wa Bandari kubwa na ya kisasa ya Bagamoyo. Amesema, awamu ya kwanza itahusisha ujenzi wa gati lenye urefu wa kilomita 1.32 ili kuwa nauwezo wa kuhudumia meli kubwa za kisasa (Mega Max).
Bandari hii inalenga kupunguza msongamano wa Bandari ya Dar es Salaam na kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha usafirishaji wa baharini Afrika Mashariki.
MRADI WA KURASINI LOGISTICS TERMINAL
Pia,Serikali imeanza utekelezaji wa Mradi wa Kurasini Logistics Terminal kwa lengo la
kupunguza msongamano wa makasha bandarini na kuboresha uhifadhi wa mizigo inayoharibika haraka (perishables)
Msigwa amesema, mradi unahusisha eneo la mita za mraba 210,000 na utakuwa na uwezo wa kuhifadhi makasha hadi 700,000 na kwa sasa Awamu ya Kwanza (mita za mraba 81,000) inaendelea kutekelezwa.
MABORESHO YA BANDARI ZA MAZIWA MAKUU
Amesema,Serikali imekamilisha maboresho ya Bandari ya Kemondo na Bandari ya Bukoba ambazo katika Ziwa Victoria zinatarajiwa kuwa kitovu cha usafirishaji kati ya Bukoba, Mwanza na bandari za Uganda, hivyo kuongeza biashara ya kikanda na kupunguza gharama za usafiri wa maji.
Kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania, Serikali inaendelea na ujenzi wa Bandari ya Kisiwa Mgao kwa ajili ya kuhudumia mizigo mchafu (Dirty Cargo) kama makaa ya mawe na saruji.
Mradi umefikia asilimia 18 ya utekelezaji ambapo kukamilika kwake kutaongeza ufanisi wa Bandari ya Mtwara na kuboresha utunzaji wa mizigo.
Kuhusu ujenzi wa Bandari ya Mbamba Bay Ziwa Nyasa amesema, mradi unahusisha gati la kuhudumia meli na shehena ya magari (RO-RO), jengo la utawala,jengo la abiria, miundombinu ya barabara na uzio ambapo mradi umefikia asilimia 46 ya utekelezaji.
Aidha,katika Ziwa Tanganyika, Serikali kupitia TPA kwa mfumo wa ubia (PPP) imekamilisha ujenzi wa meli mbili za mizigo kati ya nne zinazojengwa.
Msigwa amesema, kila meli ina uwezo wa kubeba tani 2,000 na zitachochea biashara kati ya Tanzania na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
MAFANIKIO YA MAPATO YA BANDARI
Baada ya kuingia mikataba ya ukodishaji na uendeshaji wa gati namba 17 na 811 katika Bandari ya Dar es Salaam, mapato yameongezeka kwa kiasi kikubwa.
Msigwa anasema, taarifa za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), zinzonesha kuwa mapato ya forodha kati ya Julai 2024 hadi Februari 2025 yalifikia shilingi trilioni 8.256, ikiwa ni ongezeko la shilingi trilioni 1.174 ikilinganishwa na shilingi trilioni 7.082 zilizokusanywa katika kipindi kama hicho mwaka 2023/24.
Pia,Serikali imekamilisha ujenzi wa meli ya MV New Mwanza katika Ziwa Victoria na ilizinduliwa tarehe 23 Januari, 2026 na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba.
Meli hii ina uwezo wa kubeba abiria 1,200,
mizigo tani 400, itaboresha usalama, ufanisi na huduma za usafiri katika Ziwa Victoria.
Vilevile, baada ya ukarabati mkubwa, Meli ya MT Sangara imeanza safari za kibiashara tangu Juni 2025 kwa kusafirisha mafuta kati ya Kigoma na Kalemie (DRC). Uzinduzi rasmi unatarajiwa kufanyika wakati wowote.
"Kwa ujumla, mafanikio haya yanaonesha dhamira ya dhati ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Samia Suluhu Hassan ya kuimarisha miundombinu ya bandari na usafiri majini, kuongeza mapato ya taifa na kukuza uchumi wa nchi."
USALAMA WA USAFIRI WA MAJINI NA UOKOAJI
Serikali kupitia Wizara ya Uchukuzi imeendelea kuweka kipaumbele katika kulinda maisha ya wananchi na mali zao kwa kuimarisha mifumo ya utafutaji na uokoaji majini.
Lengo ni kuhakikisha usalama wa watumiaji wa vyombo vya majini pamoja na kuwa na uwezo wa kukabiliana haraka na dharura pale zinapotokea.
Katika mwaka 2024/25 na nusu ya mwaka 2025/26,Msigwa amesema,Serikali imekamilisha ujenzi wa Kituo cha Kuratibu Utafutaji na Uokoaji cha Kikanda (Maritime Rescue Coordination Centre MRCC) katika Ziwa Victoria, Mwanza, kwa kushirikiana na Serikali ya Uganda.
Kituo hiki amesema, kitaimarisha usalama wa usafiri wa majini, uratibu wa operesheni za utafutaji na uokoaji, matumizi ya mifumo ya kisasa ya mawasiliano na TEHAMA na
utoaji wa tahadhari za hali ya hewa.
Hatua hii inaifanya Tanzania kuwa na mfumo madhubuti wa kikanda wa kukabiliana na majanga ya majini katika Ziwa Victoria.
Pia,Serikali imenunua boti maalum ya wagonjwa (Ambulance Boat) kwa ajili ya Ziwa Victoria, ambayo tayari imewasili na iko tayari kutoa huduma.
Boti hii ni kama hospitali inayotembea majini na itaboresha huduma za afya na uokoaji kwa wananchi waishio visiwani na maeneo ya mwambao.
Aidha, Serikali imenunua Boti 1 ya utafutaji na uokoaji Ziwa Tanganyika, Boti 2 Ziwa Victoria,
Boti 1 Ukanda wa Bahari ya Hindi (Tanga) ambapo hatua hii imeongeza uwezo wa Taifa katika kukabiliana na ajali na majanga ya majini.
Vilevile,wizara inaendelea na ujenzi wa minara mitatu ya mawasiliano katika Ziwa Victoria, ambapo Mnara wa Kisiwa cha Soswa umefikia asilimia 50 na Mnara wa Kisiwa cha Kunene umefikia asilimia 50.
Mradi huu unalenga kuongeza usalama wa vyombo vya majini,kuboresha mawasiliano ya dharura,kuimarisha tahadhari za hali ya hewa
na kuwezesha uratibu wa haraka wa shughuli za uokoaji.
"Serikali inapanga kutumia uzoefu uliopatikana katika Ziwa Victoria kupeleka miradi kama hii katika Ziwa Tanganyika na Ziwa Nyasa, ili kuhakikisha usalama wa usafiri wa majini unaimarika katika maziwa yote makuu nchini.
"Kwa ujumla, hatua hizi zinaonesha dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha kuwa usafiri wa majini unakuwa salama, wa kisasa na wenye uwezo wa kukabiliana na dharura kwa wakati."
MAENDELEO YA SEKTA YA UTALII NCHINI
Tanzania imebarikiwa kuwa na rasilimali nyingi za utalii zinazojumuisha vivutio vya asili, utamaduni, malikale, historia na vivutio vilivyoundwa na binadamu.
Miongoni mwa vivutio vinavyoitangaza Tanzania kimataifa ni Hifadhi ya Taifa Serengeti,Mlima Kilimanjaro,Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro,Hifadhi ya Taifa Ruaha, Hifadhi ya Taifa Mikumi na Zanzibar.
Vivutio hivi vinaifanya sekta ya utalii kuwa miongoni mwa sekta muhimu za kiuchumi nchini, yenye mchango mkubwa katika Pato la Taifa, ajira na mapato ya fedha za kigeni.
Aidha, sekta hii huchochea ukuaji wa sekta nyingine kama usafirishaji, uchukuzi, hoteli, biashara na huduma za kifedha.
MAENDELEO YA SEKTA YA UTALII NA MAFANIKIO
Sekta ya utalii imeendelea kuonesha ukuaji thabiti kama ifuatavyo:
Ongezeko la Watalii wa Nje
2024: Watalii 2,141,895
2025: Watalii 2,294,495
Ongezeko la Watalii wa Ndani
2024: Watalii 3,218,352
2025: Watalii 3,610,960
Jumla ya Watalii (Ndani na Nje)
2024: Watalii 5,360,247
2025: Watalii 5,905,455
Ongezeko: Asilimia 10.2
Mapato ya Utalii
2021: Dola za Marekani milioni 1.3
2024: Dola za Marekani milioni 3.9
Takwimu hizi zinaonesha mafanikio makubwa katika juhudi za Serikali za kukuza na kuitangaza Tanzania kama kivutio cha utalii duniani.
Ongezeko la watalii wa ndani pia linaashiria kuimarika kwa utamaduni wa utalii miongoni mwa Watanzania wenyewe.
Kwa ujumla, ukuaji huu umechangiwa na uboreshaji wa miundombinu ya usafiri (anga, reli na barabara), uwekezaji katika hifadhi za taifa na vivutio vya kihistoria na mikakati ya kimataifa ya kuitangaza Tanzania.
MAFANIKIO KATIKA SEKTA YA UTALII
Tanzania Kuendelea Kutambulika Kimataifa
Tanzania imeendelea kungara katika jukwaa la kimataifa kupitia jitihada za kuitangaza nchi kama kivutio bora cha utalii.
Mafanikio haya yamechangiwa kwa kiasi kikubwa na filamu ya Tanzania: The Royal Tour iliyoasisiwa na Samia Suluhu Hassan pamoja na filamu ya Amazing Tanzania.
Filamu hizi zimeongeza utambulisho wa Tanzania duniani na kuvutia watalii pamoja na wawekezaji katika sekta ya utalii.
Katika kipindi cha Julai hadi Desemba 2024, Tanzania ilishinda tuzo mbalimbali zinazoandaliwa na World Travel Awards kama ifuatavyo: Africas Leading Destination 2024 Tanzania, Worlds Leading Safari Destination 2024 Tanzania, Worlds Leading National Park Hifadhi ya Taifa Serengeti (ikiendelea kushinda kwa miaka sita mfululizo: 2019 2024), African Leading Tourism Attraction 2024 Mlima Kilimanjaro, Africas Leading Tourist Board Bodi ya Utalii Tanzania.
Tanzania kupata Tuzo za Dunia za WTA 2025
Katika Tuzo za Dunia za WTA zilizotolewa mwaka 2025, Tanzania ilipata ushindi katika vipengele vifuatavyo: Worlds Leading Safari Destination Tanzania,Worlds Leading National Park Hifadhi ya Taifa Serengeti,Worlds Leading Balloon Ride Operator Serengeti Balloon Safaris,Worlds Leading Exclusive Private Island Jumeirah Thanda Island, Africas Best Corporate Retreat Destination Zanzibar.
Mafanikio haya yanaonesha wazi kuwa Tanzania imeendelea kuimarisha nafasi yake kama kitovu cha utalii barani Afrika na duniani kwa ujumla.
Ushindi huu wa tuzo za kimataifa umeongeza hadhi ya nchi, kuimarisha imani ya watalii na wawekezaji, na kuchochea zaidi ukuaji wa sekta ya utalii ambayo ni mhimili muhimu wa uchumi wa taifa.
Aidha,kwa mujibu wa taarifa hiyo, mafanikio yaliyopatikana yanaakisi utekelezaji wa dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kuimarisha miundombinu ya uchukuzi na kukuza sekta za uzalishaji.
Serikali imesisitiza kuwa uwekezaji unaoendelea katika anga, reli, bandari na utalii utaendelea kuwa chachu ya ukuaji wa uchumi, ajira na ustawi wa wananchi, huku Tanzania ikiimarisha nafasi yake kama kitovu cha biashara na usafiri katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika.
