TAKUKURU yawasilisha taarifa ya utendaji kazi 2024/2025 kwa Rais Dkt.Samia

■Yaokoa shilingi bilioni 14.5, yaimarisha mapambano dhidi ya rushwa nchini

NA GODFREY NNKO

MKURUGENZI Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Bw. Crispin Francis Chalamila amewasilisha rasmi Taarifa ya Utendaji Kazi ya taasisi hiyo kwa mwaka 2024/2025 kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt.Samia Suluhu Hassan.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan akipokea Taarifa ya Mwaka ya Utendaji Kazi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi hiyo, Bw. Crispin Chalamila, Ikulu jijini Dar es Salaam tarehe 30 Machi, 2026.

Chalamila katika taarifa hiyo amebainisha mafanikio makubwa yaliyopatikana katika kuzuia na kupambana na vitendo vya rushwa nchini.

Katika hafla hiyo ambayo imefanyika leo Machi 30,2026 Ikulu jijini Dar es Salaam imehudhuriwa na viongozi wakuu wa kitaifa na viongozi wengine waandamizi wa Serikali,ambapo TAKUKURU imesisitiza dhamira yake ya kuimarisha uwajibikaji na utawala bora.

Akizungumza wakati wa uwasilishaji huo, Bw. Chalamila amesema,taarifa hiyo imewasilishwa kwa mujibu wa matakwa ya kisheria chini ya Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, Sura ya 329, kifungu cha 14, kinachoitaka TAKUKURU kuwasilisha taarifa ya utendaji kazi kila mwaka ifikapo Machi 31.
Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (TAKUKURU) Bw. Crispin Chalamila akisoma Muhtasari wa Taarifa ya Mwaka ya Utendaji Kazi wa Taasisi hiyo, Ikulu jijini Dar es Salaam, tarehe 30 Machi, 2026.

Chalamila ameeleza kuwa, katika kipindi hicho, taasisi hiyo imetekeleza majukumu yake kwa kuzingatia misingi mikuu ya kuzuia rushwa, uelimishaji wa umma, uchunguzi na uendeshaji wa mashtaka, sambamba na miongozo ya kitaifa ikiwamo Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025, Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2020/2025 na falsafa ya 4Rs.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, TAKUKURU iliweka mkazo katika maeneo matatu muhimu ambayo ni ukusanyaji wa mapato ya Serikali, udhibiti wa rushwa katika uchaguzi na utoaji wa huduma za umma, hususan sekta za afya, maji, elimu,ardhi na ujenzi.

Aidha, katika jitihada za kuzuia rushwa, TAKUKURU ilifanya tafiti mbili na uchambuzi wa mifumo 757, ikiwa ni ongezeko kutoka mwaka uliotangulia.
Viongozi pamoja na wageni mbalimbali wakiwa kwenye hafla ya kupokea Ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa Mwaka wa Fedha 2024/25, Taarifa ya Mwaka ya Utendaji Kazi wa Taasisi ya Kuzuia na kupambana na Rushwa (TAKUKURU) pamoja na Taarifa ya Mwaka ya Utendaji Kazi ya Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA), Ikulu jijini Dar es Salaam, tarehe 30 Machi, 2026.

Pia, mikakati 3,470 iliwekwa ili kuziba mianya ya rushwa, ambapo asilimia 86 ya mikakati hiyo tayari imetekelezwa.

Matokeo ya juhudi hizo, Chalamila amesema ni pamoja na kuongezeka kwa mapato ya halmashauri 40 kwa zaidi ya shilingi bilioni 8.6,kuongezeka kwa ufanisi wa ukusanyaji wa mapato kwa kutumia mashine za kielektroniki (POS) na urejeshwaji wa kodi ambazo hazikukatwa awali na kuwasilishwa kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Vilevile, TAKUKURU ilifuatilia miradi ya maendeleo 1,864 yenye thamani ya shilingi trilioni 14.3. Kati ya miradi hiyo, 913 ilibainika kuwa na kasoro, huku miradi 66 ikianzishiwa uchunguzi.
Amesema,changamoto zilizobainika ni pamoja na usimamizi dhaifu wa mikataba,malipo kwa kazi zisizotekelezwa,ukiukwaji wa taratibu za ununuzi wa umma, ubora hafifu wa kazi na vifaa.

Katika kuhamasisha jamii kushiriki mapambano dhidi ya rushwa, Bw.Chalamila amesema taasisi hiyo ilifanya semina 4,760, mikutano ya hadhara 4,143, maonesho 544 na uimarishaji wa klabu za wapinga rushwa 7,042.

Amesema, jumla ya wanachama wa klabu hizo ilifikia 996,807, ikiwa ni ongezeko kubwa kutoka mwaka uliopita.

Bw.Chalamila amefafanua kuwa, uelewa wa wananchi kuhusu rushwa uliongezeka hadi asilimia 84.6 mwaka 2024 kutoka asilimia 77.5 mwaka 2020.
Viongozi pamoja na wageni mbalimbali wakiwa kwenye hafla ya kupokea Ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa Mwaka wa Fedha 2024/25, Taarifa ya Mwaka ya Utendaji Kazi wa Taasisi ya Kuzuia na kupambana na Rushwa (TAKUKURU) pamoja na Taarifa ya Mwaka ya Utendaji Kazi ya Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA), Ikulu jijini Dar es Salaam, tarehe 30 Machi, 2026.
Kupitia operesheni mbalimbali za uchunguzi, amesema TAKUKURU ilifanikiwa kuokoa kiasi cha Shilingi bilioni 14.5. 

Kati ya fedha iliyookolewa, Shilingi bilioni 10.1 ni fedha taslimu ambayo iliwekwa kwenye akaunti za Taasisi na Idara za Serikali na Shilingi bilioni 4.4 ilidhibitiwa sambamba na kurejesha vifaa na mali zilizoelekezwa kwenye utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Miongoni mwa maeneo yaliyochangia uokoaji huo ni ushuru wa huduma uliolipwa na kampuni mbalimbali,mikopo ya vyama vya ushirika iliyorejeshwa na mapato ya viwanja yaliyokuwa hayajalipwa ipasavyo.

Katika kipindi hicho, amesema majalada 1,030 ya uchunguzi yalikamilika, yakiwamo 22 ya rushwa kubwa yenye thamani ya shilingi bilioni 210.5.
Viongozi pamoja na wageni mbalimbali wakiwa kwenye hafla ya kupokea Ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa Mwaka wa Fedha 2024/25, Taarifa ya Mwaka ya Utendaji Kazi wa Taasisi ya Kuzuia na kupambana na Rushwa (TAKUKURU) pamoja na Taarifa ya Mwaka ya Utendaji Kazi ya Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA), Ikulu jijini Dar es Salaam, tarehe 30 Machi, 2026.
Kwa upande wa mashtaka amesema, kesi 1,016 ziliendeshwa mahakamani, kesi 593 zilitolewa uamuzi na kesi 483 zilishindwa na Jamhuri kushinda asilimia 81.5 ya kesi zote.

Amefafanua kuwa, TAKUKURU iliendelea kushirikiana na wadau wa ndani na kimataifa, wakiwamo asasi za kiraia, vyombo vya dola, vyama vya siasa na taasisi za kimataifa kupitia mikataba mbalimbali ya kupambana na rushwa.

Pia, taasisi hiyo kwa kushirikiana na Taasisi ya Elimu Tanzania inaendelea kuingiza maudhui ya mapambano dhidi ya rushwa katika mitaala ya elimu.
Viongozi pamoja na wageni mbalimbali wakiwa kwenye hafla ya kupokea Ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa Mwaka wa Fedha 2024/25, Taarifa ya Mwaka ya Utendaji Kazi wa Taasisi ya Kuzuia na kupambana na Rushwa (TAKUKURU) pamoja na Taarifa ya Mwaka ya Utendaji Kazi ya Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA), Ikulu jijini Dar es Salaam, tarehe 30 Machi, 2026.
Kwa mwaka ujao wa fedha, Bw.Chalamila amesema,TAKUKURU imepanga kuimarisha juhudi zake katika maeneo ya udhibiti wa ruzuku katika halmashauri, ukusanyaji wa mapato ya Serikali,utoaji wa huduma za jamii, ushirikiano na wadau.

Bw. Chalamila amemshukuru Rais Dkt.Samia kwa kuendelea kuimarisha taasisi hiyo kupitia ongezeko la bajeti, ununuzi wa vifaa, mafunzo kwa watumishi na uboreshaji wa miundombinu ya ofisi.
Viongozi pamoja na wageni mbalimbali wakiwa kwenye hafla ya kupokea Ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa Mwaka wa Fedha 2024/25, Taarifa ya Mwaka ya Utendaji Kazi wa Taasisi ya Kuzuia na kupambana na Rushwa (TAKUKURU) pamoja na Taarifa ya Mwaka ya Utendaji Kazi ya Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA), Ikulu jijini Dar es Salaam, tarehe 30 Machi, 2026.
Amesisitiza kuwa,TAKUKURU itaendelea kusimamia sheria bila upendeleo na kuhakikisha wahusika wa vitendo vya rushwa wanachukuliwa hatua kali za kisheria.

Bw.Chalamila amemkabidhi rasmi nakala za taarifa hiyo kwa Rais, akiahidi kuwa taasisi hiyo itaongeza juhudi katika kulinda rasilimali za umma na kuhakikisha uwajibikaji unaimarika nchini.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here