NEW DELHI-Tanzania na India zimeendelea kusisitiza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano wa kihistoria na kindugu kuliopo baina ya mataifa hayo mawili.
Hayo yamejadiliwa katika mazungumzo kati ya Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Ngwaru Maghembe na Waziri wa Mambo ya Nje wa India, Mhe. Dkt. Subrahmanyam Jaishankar yaliyofanyika jijini New Delhi, India, Machi 6, 2026.
Katika mazungumzo yao, viongozi hao walikubaliana kuendeleza ushirikiano katika sekta za kimkakati kama maji, kilimo, teknolojia, afya, uchumi wa buluu, uchukuzi, biashara na uwekezaji.
Awali akizungumza, Mhe. Dkt. Maghembe aliishukuru India kwa kuwa mshirika muhimu wa maendeleo wa Tanzania na kupongeza ukuaji wa biashara kati ya nchi hizo. Pia aliwahimiza wawekezaji kutoka India kuja kuwekeza zaidi nchini, akitaja fursa zilizopo katika kuongeza thamani ya mazao ya kilimo kama korosho, alizeti, michikichi na bidhaa za ngozi pamoja na uwekezaji kupitia ubia wa sekta ya umma na binafsi (PPP).
Kwa upande wake, Dkt. Jaishankar alieleza kuridhishwa na ukuaji wa ushirikiano kati ya India na Tanzania, akisema umechangia kuongezeka kwa biashara na uwekezaji baina ya nchi hizi mbili.
India ni miongoni mwa washirika wakubwa wa biashara wa Tanzania, huku pia ikiwa imewekeza zaidi ya miradi 600 iliyotoa ajira za moja kwa moja kwa Watanzania zaidi ya 60,000.
Mhe. Dkt. Maghembe yupo nchini India kwa ziara ya kikazi na kushiriki Mkutano wa Jukwaa la Raisina 2026 kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo.



