DAR-Tanzania na Uganda zimekutana kupitia maeneo ya ushirikiano wa maendeleo ya pamoja ya kiuchumi na kijamii kati ya nchi hizo mbili rafiki, katika Mkutano wa Tano (5) wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano (JPC) Machi 11, 2026.
Hatua hiyo imekuja kufuatia majadiliano yaliyofanyika wakati wa JPC hiyo, pande hizo mbili zimeanisha makundi manne ya maeneo ya ushirikiano wa kimkakati katika kufanikisha maazimio ya ukuaji wa pamoja wa kimaendeleo.
Majadiliano hayo ya wataalamu yanatarajiwa kuweka msingi wa maamuzi yatakayofikiwa katika vikao vya ngazi ya maafisa waandamizi na hatimaye kikao cha mawaziri kitakachohitimisha mkutano huo wa JPC hapo Machi 13, 2026.
Eneo la kwanza ni la Ushirikiano wa Kidiplomasia, Kisiasa, Ulinzi na Usalama, Masuala ya Kisheria na Uhamiaji. Eneo la pili ni la Maendeleo ya Miundombinu (Ujenzi, Uchukuzi na Nishati).
Aidha, eneo la tatu ni kuhusu Masuala ya Kiuchumi (Biashara na Viwanda, Mifugo na Uvuvi, Kilimo, Maji, Mazingira na Utalii) na mwisho ni Masuala ya Kijamii.
Kupitia ushirikiano huo wa kimkakati, Tanzania na Uganda zinatarajia kupanua zaidi fursa za kibiashara na uwekezaji, kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia uliodumu kwa muda mrefu, pamoja na kuchochea maendeleo ya kitaifa na kikanda.
Wawakilishi kutoka wizara, taasisi na idara mbalimbali za kiserikali za Tanzania na Uganda wameshiriki JPC hiyo kwa lengo la kupitia utekelezaji wa makubaliano yaliyofikiwa katika JPC ya nne mwaka 2022 na kuweka maazimio mapya katika mkutano wa sasa.

















