DAR-Wafanyakazi watano wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ni miongoni mwa wahitimu 158 wa Mpango wa Kuandaa Viongozi Wanawake wa Baadaye-Kundi la 11, ulioandaliwa na Chama cha Waajiri Tanzania (ATE), katika hafla ya mahafali iliyofanyika tarehe 4 Machi 2026.
Ushiriki wa wafanyakazi hao unaakisi dhamira ya BoT katika kuwawezesha wanawake kwa kuwapatia ujuzi wa uongozi pamoja na fursa za maendeleo ya kitaaluma.
Mafanikio hayo yanaonesha pia kuongezeka kwa uungwaji mkono wa taasisi kwa mipango inayochochea uongozi wa wanawake na kukuza maendeleo yao ya kitaaluma nchini.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mgeni Rasmi, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Mussa Hassan Nzungu, aliwapongeza wahitimu kwa kukamilisha mafunzo yao na kuipongeza ATE kwa juhudi zake endelevu za kuandaa na kukuza viongozi wanawake wa baadaye.
Alisisitiza kuwa uwezeshaji wa wanawake ni muhimu katika kukuza uchumi jumuishi na kuharakisha maendeleo endelevu ya taifa. Aidha, aliwahimiza wahitimu kutumia maarifa na ujuzi walioupata kupitia mpango huo kuleta mabadiliko chanya katika taasisi na sekta wanazofanyia kazi.
Mpango wa Kuandaa Viongozi Wanawake wa Baadaye unaotekelezwa na ATE ni mpango wa miezi tisa unaolenga kuwajengea wanawake wanaochipukia katika uongozi uwezo wa vitendo wa uongozi, ushauri wa kitaaluma pamoja na fursa za kujenga mitandao ya kitaaluma.
Kupitia mafunzo, majadiliano ya pamoja na ushiriki katika shughuli mbalimbali za kitaaluma, washiriki hujengewa kujiamini na uwezo wa kuongoza kwa ufanisi ndani ya taasisi zao na katika jamii.
Hafla hiyo ilihitimishwa kwa kuwatambua rasmi wahitimu kwa kukamilisha kwa mafanikio mpango huo na kuwakaribisha kujiunga na mtandao mpana unaokua wa wanawake viongozi waliowezeshwa, wenye dhamira ya kuchangia maendeleo ya taasisi zao na ya taifa kwa ujumla.
