DAR-Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb) ameipongeza, Kampuni ya Mawasiliano ya Airtel Tanzania kwa mchango wake katika kukuza sekta ya mawasiliano nchini na kuitaka iongeze uwekezaji katika miundombinu na huduma za mawasiliano ya kidijitali ili kuendana na malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050.
Mhe. Omar amesema hayo katika tukio la Iftar lililoandaliwa na Kampuni hiyo kwa wateja wake na makundi mengine ya kijamii lilofanyika katika Hoteli ya Serena jijini Dae Salaam.
Alisema kuwa,Airtel Tanzania ni miongoni mwa kampuni kubwa za mawasiliano nchini ambazo zimeendelea kuwa washirika muhimu wa Serikali katika kuendeleza huduma za mawasiliano na teknolojia ya habari.
Mhe. Balozi Omar, aliitaka Airtel Tanzania kuendelea kuongeza uwekezaji katika sekta ya mawasiliano, ili iweze kuchangia kwa kiwango kikubwa zaidi katika ukuaji wa uchumi na utekelezaji wa malengo ya Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050.
“Katika kutekeleza Dira Mpya ya Taifa ya Maendeleo ya 2050, Tanzania inatakiwa kuwa na uchumi wa dola za Marekani trilioni moja ifikapo kwa huo, ambapo asilimia 70 ya fedha hizo zinatakiwa kuchangiwa na Sekta Binafsi, huku Serikali ikitakiwa kuchangia asilimia 30 ambazo ndani yake kuna asilimia 8 zinazotarajiwa kukusanywa kutoka katika mashirika na taasisi za umma,” alisema Mhe.Balozi Omar.
Aliahidi kwa upande wake kwamba Serikali itaendelea kushirikiana na sekta binafsi kwa kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara na uwekezaji kwa faida ya pande zote mbili ili malengo hayo yaweze kufikiwa.
Kwa upande wake Afisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Airtel Tanzania, Bw. Chrles Kamoto alisema kuwa, kampuni hiyo imeendelea kutoa mchango mkubwa katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii hapa nchini ambapo inawahudumia zaidi ya wateja milioni 25.
Alisema kuwa,kupitia uwekezaji wa miundombinu ya mawasiliano ya kidigitali kila kona ya nchi hii, Airtel Tanzania imechangia kuwaunganisha Wateja wanaopata huduma Jumuishi za kifedha ambazo zimechangia kurahisisha ufanyaji miamala na kuchochea biashara na shughuli nyingine za kiuchumi.











