NA DIRAMAKINI
SERIKALI ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imetangaza kwa masikitiko makubwa kifo cha aliyekuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), Mheshimiwa William Vangimembe Lukuvi kilichotokea leo Machi 25,2026.
Kwa mujibu wa taarifa rasmi iliyotolewa na Ikulu, Mheshimiwa Lukuvi amefariki dunia majira ya saa moja asubuhi katika Hospitali ya Benjamin Mkapa iliyopo jijini Dodoma, alipokuwa akipatiwa matibabu kufuatia maradhi ya mshtuko wa moyo.
Marehemu Lukuvi pia alikuwa Mbunge wa Jimbo la Isimani, ambapo alihudumu kwa muda mrefu akiwakilisha wananchi wake na kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo ya taifa.
Enzi za uhai wake, alitambulika kwa mchango wake mkubwa katika utumishi wa umma na uongozi wa serikali katika sekta mbalimbali.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, ametoa salamu za pole kwa familia ya marehemu, Spika wa Bunge, wananchi wa Jimbo la Isimani, ndugu, jamaa na Watanzania wote kwa ujumla kufuatia msiba huo mzito.
Serikali imesema itaendelea kutoa taarifa zaidi kuhusu taratibu za mazishi mara zitakapokamilika.
Kifo cha Mheshimiwa Lukuvi ni pigo kubwa kwa taifa, kikiacha pengo katika uongozi na utumishi wa umma nchini. Mwenyezi Mungu ailaze roho ya marehemu mahali pema peponi.


