NA DIRAMAKINI
MDHIBITI na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) amebaini kuwa, licha ya asilimia 99 ya taasisi za umma kupata hati safi za ukaguzi kwa mwaka wa fedha 2024/25, bado kuna changamoto kubwa katika usimamizi wa rasilimali, utekelezaji wa miradi na utoaji wa huduma katika sekta mbalimbali.
Ripoti hizo zimewasilishwa kwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, Machi 30, 2026 na baadaye kuwasilishwa rasmi bungeni Aprili 10, 2026 kwa mujibu wa Ibara ya 143 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi (NAOT) leo Aprili 14,2026, jumla ya kaguzi 1,554 zilifanyika, ambapo kati ya kaguzi 1,339 za taarifa za fedha, asilimia 99 zilipata hati safi, hali inayoashiria kuimarika kwa uandaaji wa hesabu na uzingatiaji wa kanuni za kifedha.
Hata hivyo, CAG ameonya kuwa hati safi haimaanishi kutokuwepo kwa dosari, akisisitiza kuwa bado kuna udhaifu katika mifumo ya udhibiti wa ndani na utoaji wa huduma kwa wananchi.
Ripoti hiyo imeainisha kuwa, asilimia 1 ya taasisi zilipata hati zisizoridhisha, zikiwemo hati zenye shaka, hati mbaya na kushindwa kutolewa kwa maoni kutokana na ukosefu wa ushahidi wa kutosha wa ukaguzi.
Hali hii inaonesha kuwepo kwa mapungufu makubwa katika baadhi ya taasisi, hususan katika usimamizi wa fedha na uendeshaji wa shughuli zake.
Katika tathmini ya utekelezaji wa mapendekezo ya ukaguzi, ripoti imeonesha kuwa ni asilimia 36.7 tu ya mapendekezo 38,181 yaliyotolewa katika miaka iliyopita ndiyo yametekelezwa kikamilifu.
Aidha, baadhi ya mapendekezo yamedumu bila utekelezaji kwa kipindi cha hadi miaka 20, hali inayotafsiriwa kuwa ni udhaifu wa muda mrefu katika uwajibikaji na ufuatiliaji wa masuala ya msingi.
Katika sekta ya afya, ukaguzi umebaini changamoto katika ununuzi na usambazaji wa dawa, ikiwemo uwepo wa dawa zilizokwisha muda wake na vifaa tiba visivyotumika ipasavyo.
Sekta ya elimu nayo imeendelea kukabiliwa na upungufu wa miundombinu, uhaba wa vifaa vya kujifunzia na ucheleweshaji wa miradi ya maendeleo.
Kwa upande wa maji, kiwango cha maji yasiyoingiza mapato kimebaki juu kwa wastani wa asilimia 35 kutokana na miundombinu chakavu, uvujaji na maunganisho haramu.
Nishati na miundombinu yakumbwa na changamoto
Pia,katika sekta ya nishati, changamoto zilizobainika ni pamoja na ucheleweshaji wa miradi, kuongezeka kwa gharama na madeni, pamoja na usimamizi dhaifu wa mikataba.
Aidha, miradi ya miundombinu, ikiwemo barabara na viwanja vya michezo, imeendelea kukumbwa na ucheleweshaji, gharama kubwa na ubora usioridhisha wa kazi, hali inayochangiwa na usimamizi hafifu wa mikataba na malipo kwa wakandarasi.
CAG pia amebainisha kuwepo kwa changamoto katika usimamizi wa fedha, ikiwemo kutofuata taratibu za ununuzi, ukusanyaji hafifu wa mapato na utegemezi wa ruzuku kwa baadhi ya mashirika ya umma.
Katika mifumo ya TEHAMA, ripoti imeonesha kuwa bado kuna ukosefu wa muunganiko wa mifumo ya serikali, marudio ya majukumu na matumizi ya mifumo nje ya utaratibu rasmi, hali inayodhoofisha uwajibikaji na ufanisi.
Kwa upande wa maeneo mapya ya mapato, ripoti imeeleza kuwa, Tanzania bado haijanufaika kikamilifu na biashara ya kaboni licha ya kuwa na rasilimali kubwa za misitu na mikoko.
Changamoto zilizobainika ni pamoja na mikataba isiyo na masharti madhubuti, mifumo dhaifu ya ufuatiliaji na ukosefu wa mapato ya maana katika sekta hiyo.
Pamoja na changamoto hizo, ripoti imeonesha mafanikio kadhaa, ikiwemo kuongezeka kwa hati safi za ukaguzi na kuimarika kwa ukusanyaji wa mapato ya ndani, uliovuka asilimia 99 ya malengo.
Kutokana na matokeo hayo, CAG amependekeza kuimarishwa kwa usimamizi wa miradi na mikataba, mifumo ya uwajibikaji, ukusanyaji wa mapato na matumizi ya TEHAMA, pamoja na kuhakikisha utekelezaji wa mapendekezo ya ukaguzi unafanyika kwa wakati.
Ripoti hizo sasa zinapatikana kwa umma kupitia tovuti ya Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi pamoja na majukwaa rasmi ya mawasiliano ya Serikali.
