NA DIRAMAKINI
KAMANDA wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Jumanne Murilo amesema, hali ya usalama katika jiji hilo kwa sasa ni shwari, akieleza kuwa mafanikio hayo yanatokana na jitihada za pamoja kati ya Jeshi la Polisi na wananchi.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Aprili 27,2026 Kamnda Murilo amebainisha kuwa, utulivu huo unatofautiana na hali iliyokuwapo katika baadhi ya siku za nyuma, huku akisisitiza kuwa ushirikiano wa karibu kati ya vyombo vya dola na jamii umeimarisha kwa kiasi kikubwa udhibiti wa vitendo vya uhalifu.
Amesema, Jeshi la Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam linaendelea kuzuia na kudhibiti uhalifu kwa kutumia taarifa za kiintelijensia zinazotolewa na wananchi pamoja na wadau wengine wa usalama.
Ameongeza kuwa, mchango wa jamii umekuwa nyenzo muhimu katika kubaini na kufuatilia wahalifu.
Katika hatua nyingine, Kamanda Murilo amesema kuwa mnamo Aprili 20, 2026, polisi walifanikiwa kuwakamata watu 37 katika eneo la Ubungo kwa tuhuma za kujihusisha na makosa ya kimtandao, yakiwemo utoaji wa vitisho na matumizi ya lugha chafu dhidi ya watu mbalimbali kupitia majukwaa ya kidijitali.
Amefafanua kuwa,uchunguzi wa awali umebaini kuwa baadhi ya watuhumiwa hao ni wafanyakazi wa kampuni za INNOVIX CALL CO LTD na OTAIGO FINANCIAL SERVICES COMPANY LIMITED, ambazo zinajihusisha na utoaji wa mikopo kwa njia ya mtandao.
Miongoni mwa waliotajwa ni Renatus Mujwahuzi maarufu kama “Migeyo”, mkazi wa Mbezi Beach; Odilia Oswin “Ngunga”, mkazi wa Goba Njia Nne; pamoja na Theresia Brastius “Kanu”, mkazi wa Mtoni Kijichi, sambamba na wenzao 34.
“Hatua zaidi zinaendelea kuchukuliwa ili kuwafikisha watuhumiwa hao katika vyombo husika vya kisheria kwa hatua stahiki,” amesema Murilo.
Aidha, Kamanda huyo amepongeza wananchi na wadau wa usalama kwa kuendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi katika kuhakikisha watuhumiwa wa vitendo vya uhalifu wanakamatwa na kufikishwa katika mifumo ya haki jinai kwa mujibu wa sheria.
Akizungumzia takwimu za utekelezaji wa sheria kwa kipindi cha Machi hadi Aprili 2026, Murilo amesema mahakama mbalimbali jijini Dar es Salaam zimetoa hukumu kwa watuhumiwa waliopatikana na hatia katika makosa mbalimbali mazito.
Miongoni mwa waliohukumiwa ni Hashimu Kasimu maarufu kama “Duma”, mkazi wa Kimara, aliyepatiwa kifungo cha maisha na Mahakama ya Wilaya ya Ubungo kwa kosa la ulawiti.
Vivyo hivyo, Vicent Laurent “Ndimbo”, mkazi wa Urafiki Kinondoni, alihukumiwa kifungo cha maisha na Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni kwa kosa la ubakaji.
Kwa upande mwingine, Habibu Nassoro na Ismail Ally “Muro”, wote wakazi wa Charambe, walihukumiwa na Mahakama ya Wilaya ya Temeke kifungo cha maisha na miaka 30 mtawalia kwa makosa ya ulawiti na ubakaji.
Nelson Julius wa Mavurunza Kimara naye alihukumiwa kifungo cha miaka 30 jela kwa kosa la unyang’anyi wa kutumia silaha na Mahakama ya Wilaya ya Ubungo.
Wengine ni Fadhili Issa, Peniel Jonathan “Mtakibaleza” na Yusuph Iddi, wote wakazi wa Mbagala, ambao walihukumiwa kifungo cha miaka 30 jela kwa makosa ya ubakaji, huku Iddi akikutwa na hatia ya kubaka na kumpa mimba mwanafunzi.
Kamanda Murilo ametoa wito kwa wananchi kuendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi kwa kutoa taarifa za viashiria vya uhalifu kwa wakati, ili ziweze kufanyiwa kazi haraka.
Pia amesisitiza umuhimu wa wananchi kujitokeza mahakamani kutoa ushahidi utakaosaidia kuhakikisha haki inatendeka.
Amesema,ushirikiano huo ni msingi muhimu katika kudumisha amani na usalama endelevu katika Jiji la Dar es Salaam.
Tags
Dar es Salaam City
Habari
Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam
Jeshi la Polisi Tanzania
Ulinzi na Usalama
