Kutoka nyumbani hadi darasani,polisi wabadilisha hatma ya mwanafunzi Iramba

SINGIDA-Jeshi la Polisi katika Kata ya Mtoa, Wilaya ya Iramba mkoani Singida limefanikiwa kumrejesha shuleni mwanafunzi mmoja aliyekuwa ameacha masomo, ikiwa ni sehemu ya mkakati endelevu wa kukabiliana na tatizo la utoro shuleni na kuhamasisha elimu kwa watoto.
Mafanikio hayo yamepatikana Aprili 27, 2026, yakiongozwa na Mkaguzi Msaidizi wa Polisi (A/INSP),Aamari Kidagaa, baada ya kufika katika Kijiji cha Tyeme kufuatilia kwa kina sababu zilizopelekea mwanafunzi huyo, Grace Jacob, kusitisha masomo yake.

Ziara hiyo ilikuwa na lengo la kubaini changamoto za kifamilia na kijamii zinazoathiri maendeleo ya elimu kwa watoto, sambamba na kutoa elimu kwa wazazi kuhusu wajibu wao katika kuhakikisha watoto wanapata haki ya msingi ya elimu.

Akizungumza na familia ya mwanafunzi huyo, A/INSP Kidagaa alisisitiza umuhimu wa elimu si tu kwa maendeleo ya mtoto binafsi, bali pia kwa ustawi wa familia, jamii na Taifa kwa ujumla.

Alieleza kuwa, uwekezaji katika elimu ni msingi imara wa kujenga rasilimali watu yenye tija, hivyo ni wajibu wa kila mzazi na mlezi kuhakikisha watoto wanapata fursa hiyo bila vikwazo.

Baada ya mazungumzo hayo, baba mzazi wa mwanafunzi huyo, Bw. Jacob Narogwa, alikiri kuwepo kwa changamoto zilizochangia mtoto wake kushindwa kuendelea na masomo, na kuahidi kushirikiana na mamlaka husika ili kuhakikisha binti yake anarejea shuleni haraka iwezekanavyo.

Aidha, alimshukuru Askari huyo wa Polisi kwa juhudi za kuwafikia wananchi moja kwa moja na kutoa elimu yenye tija kwa jamii.

Bw. Narogwa pia aliwataka wazazi na walezi wengine kuiga mfano huo kwa kuthamini elimu ya watoto wao, huku akiomba elimu hiyo iendelee kutolewa kwa jamii pana ili kupunguza tatizo la utoro na kuongeza kiwango cha uandikishaji na mahudhurio shuleni.

Hatua hiyo inaakisi dhamira ya Jeshi la Polisi kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya jamii kwa kushirikiana na wananchi, si tu katika kudumisha usalama na utulivu, bali pia katika kukuza ustawi wa kijamii kupitia elimu.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here