NA DIRAMAKINI
MREMBO Latricia Ian ametwaa taji la Miss Tanzania 2026 katika shindano lililofanyika usiku wa Jumamosi, Aprili 19, katika ukumbi wa Super Dome, jijini Dar es Salaam, likihudhuriwa na wageni mbalimbali waalikwa pamoja na wapenzi wa tasnia ya urembo na burudani.
Patricia aliibuka mshindi baada ya kuonesha kiwango cha juu cha ushindani kuanzia hatua za awali hadi fainali, akiwashinda washiriki wenzake hususan katika hatua ya mwisho ya maswali na majibu, ambapo alijibu kwa ufasaha na kuonyesha kujiamini.
Kabla ya ushindi huo wa kitaifa, Latricia aliwahi kushika nafasi ya tatu katika shindano la Miss Dar es Salaam, hatua iliyomjengea uzoefu uliomuwezesha kufanya vizuri zaidi katika jukwaa la taifa.
Aidha, katika hafla hiyo ya kifahari, Latricia alivishwa taji na mshindi wa Miss World 2025, Opal Suchata kutoka Thailand, aliyekuwa mgeni rasmi.
Sambamba na Miss World Africa 2025 pamoja na mkurugenzi wa Miss World, waliokuwa nchini Tanzania kwa shughuli hiyo maalum.
Kwa ushindi huo, Latricia amejinyakulia zawadi ya gari, fedha taslimu, pamoja na jukumu la kuiwakilisha Tanzania katika shindano la Miss World litakalofanyika nchini Vietnam baadaye mwaka huu.
Usiku huo ulipambwa na burudani kutoka kwa wasanii maarufu, akiwemo nyota wa muziki wa Bongo Flava, Alikiba, pamoja na mwanamuziki wa asili, Wanne Star, waliotoa burudani iliyoongeza shamrashamra ukumbini.
Majaji wa shindano hilo walijumuisha majina yenye uzoefu mkubwa katika tasnia, akiwemo Rita Paulsen maarufu kama Madame Rita, Issa Muhdini Michuzi mwenye historia ndefu ya kushiriki katika shughuli za Miss Tanzania tangu enzi za Hashim Lundenga.
Pamoja na Mbiki Msumi na Doris Mollel, ambao wote waliwahi kushika nafasi za juu katika mashindano ya Miss Tanzania ya miaka ya nyuma.
Miongoni mwa wageni rasmi waliohudhuria hafla hiyo ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Gerson Msigwa, ambaye pia ni Msemaji Mkuu wa Serikali.
Ushindi wa Latricia Ian unaashiria mwanzo mpya wa safari yake katika jukwaa la kimataifa, huku Watanzania wakitarajia kuona uwakilishi madhubuti katika mashindano ya dunia yajayo.
